Na Matukio Daima Media, Iringa
Mbunge aliyemaliza muda wake wa Jimbo la Ismani, William Vangimembe Lukuvi, ameibuka mshindi wa kishindo katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya ubunge wa jimbo hilo, akiwashinda wagombea wenzake kwa tofauti kubwa ya kura.
Huku wananchi wa Kihorogota na Kising'a wakieleza kuwa ushindi wa Lukuvi ni ishara tosha kuwa Oktoba wanatiki kwa uzido huo kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan .
"Tunataka kuonesha watu wanaosema wamekuja kumstafisha Lukuvi ubunge kuwa sisi wananchi bado tunamuitaji Lukuvi wetu kazi kubwa ameishanya jimboni hata kama wao wanadai ni mzee basi sisi ni mzazi wetu tunae na tunatamba nae "
Katika matokeo yaliyotangazwa rasmi kutoka kata zote 13 za Jimbo la Ismani, Lukuvi amepata jumla ya kura 5,746 huku mpinzani wake wa karibu, Festo Kiswaga, akipata kura 1,159 tu.
Tofauti ya kura baina yao ni kura 4,587, hali inayoonesha jinsi wanachama wa CCM katika jimbo hilo walivyomuamini Lukuvi kuendelea kuwa mwakilishi wao.
Katika kata ya Mahuninga, Lukuvi alipata kura 421 dhidi ya Kiswaga aliyepata kura 28. Hali kama hiyo ilijirudia katika kata ya Malenga Makali ambako Lukuvi alipata kura 464 huku Kiswaga akipata 139. Kata ya Migoli ilimpa Lukuvi kura nyingi zaidi—kura 644, huku Kiswaga akijikusanyia kura 84.
Kwenye kata ya Kihorogota, Lukuvi alipata kura 431 dhidi ya 63 za Kiswaga. Kata ya Kising’a Lukuvi alipata 448, huku Kiswaga akipata 40.
Kata nyingine kama Izazi, Mboliboli, Itunundu na Ilolo Mpya pia zilimpa ushindi wa kushangaza, akizidiwa tu kwa ukaribu katika kata ya Mlowa ambapo alipata kura 350 huku Kiswaga akiwa naye karibu kwa kura 340.
Kata ya Idodi ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyompa Lukuvi kura nyingi zaidi, akipata kura 676 dhidi ya 26 za Kiswaga, wakati kata ya Mlenge ilimpa Lukuvi kura 610 huku Kiswaga akipata 200. Kata ya Nyang’oro Lukuvi alipata kura 461 dhidi ya 90 za Kiswaga.
Ushindi huu wa Lukuvi unadhihirisha namna ambavyo bado ana ushawishi mkubwa ndani ya chama na kwa wananchi wa Jimbo la Ismani.
Wananchi wengi wamekuwa wakimuelezea Lukuvi kama kiongozi mwenye maono, anayejua changamoto za eneo hilo na mwenye uzoefu wa kutosha katika siasa za kitaifa na maendeleo ya jamii.
Kwa ushindi huu mkubwa, Lukuvi anatarajiwa kupeperusha tena bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao iwapo chama kitampitisha , huku matarajio ya wananchi wake yakiwa ni kuona kasi ya maendeleo inaendelezwa pale ilipoishia.
Ushindi wa Lukuvi umepongezwa na wapiga kura wengi wa kata hizo huku wakidai matusi na vijembe vya wagombea kwake viliwakwaza wajumbe ambao wamekuwa wakiheshimu mchango wa Lukuvi katika maendeleo ya jimbo hilo.
0 Comments