Na Chausiku said
Matukio Daima Mwanza.
Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema Tanzania inaweza kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 endapo itawekeza katika rasilimali watu, nafasi ya kijiografia na diplomasia ya kiuchumi.
Kafulila ameeleza kuwa nguvu kazi, maarifa na ujuzi wa kisasa ndiyo msingi wa uchumi imara, ikisaidia taifa kushindana na kuzalisha kwa tija kubwa.
Alibainisha pia kuwa nafasi ya kijiografia ya Tanzania ni fursa ya kipekee kwa kuwa inapakana na mataifa mengi yasiyo na bandari, hivyo kufungua milango ya biashara kimataifa kupitia bahari. “Zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani inapita majini, na hii ni nafasi tunayopaswa kuitumia kwa uwekezaji mkubwa katika bandari,” alisema.
Kwa mujibu wake, hatua za Serikali kushirikisha sekta binafsi kwenye miradi kama bandari ya Bagamoyo na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mapato na ushindani wa kibiashara.
Akizungumzia diplomasia ya kiuchumi, Kafulila alisema mageuzi ya Serikali ya awamu ya sita yamechochea ongezeko la thamani ya biashara za kimataifa za Tanzania kutoka dola milioni 17 mwaka 2021 hadi zaidi ya dola milioni 34, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya kitaifa.
0 Comments