Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Bodi ya Jukwaa la Ufugaji Nyuki Tanzania (TABEDO) imemtembelea Waziri Mkuu mstaafu na mlezi wa jukwaa hilo, Mhe. Mizengo Pinda, jijini Dodoma leo, kwa lengo la kutoa tathmini ya utekelezaji wa shughuli zake na kuomba ushirikiano zaidi ili kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki nchini.
Akisoma taarifa ya Bodi, Katibu wa TABEDO, Bi. Catherine Peter, alisema jukwaa hilo, lililosajiliwa mwaka 2015 chini ya Sheria ya Makampuni (Companies Act, 2002 Cap. 2012), lina jukumu la kuwaunganisha wadau wa nyuki nchini wakiwemo wafugaji, wachakataji, wafanyabiashara wa mazao, wasambazaji wa vifaa, watafiti na wanazuoni.
“Tumejipanga kuimarisha mtandao wa wadau, kuhamasisha na kutetea masilahi yao, pamoja na kuwakilisha sekta katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, tunashirikiana na Serikali katika mapitio ya sera na kanuni zinazohusu ufugaji nyuki,” alisema Bi. Peter.
Aidha, alisema TABEDO imeweka kipaumbele katika kuhamasisha wafugaji nyuki pamoja na wadau wote waliopo katika mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki kujiunga na jukwaa hilo, ili kuimarisha nguvu ya pamoja ya sekta.
Tangu mwaka 2022, TABEDO imetekeleza miradi na shughuli mbalimbali ikiwemo vikao vya wadau, kuanzisha Mfumo Shirikishi wa uratibu wa kisekta, kuandaa Mpango Mkakati wa 2023–2027, kufanya uchaguzi wa Bodi mpya, kushiriki maonesho ya kitaifa kama Saba Saba na Nane Nane, na kutoa mafunzo ya uongozi kwa wajumbe wake.
Jukwaa limeomba msaada wa mlezi wake katika upatikanaji wa kiwanja jijini Dodoma kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kudumu cha ofisi, mafunzo na mikutano, pamoja na kusaidia uimarishaji wa mfumo wa kidijitali wa kusajili wanachama (Integrated Members Management System – IMMS).
Kwa upande wake, Mhe. Pinda alilipongeza jukwaa hilo kwa hatua kubwa zilizopigwa na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mtandao wa uongozi, kutoa kipaumbele kwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya nyuki kama Kigoma, Katavi, Tabora na Dodoma, na kuendeleza ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Alisisitiza pia umuhimu wa TABEDO kupanua uwakilishi wake hadi ngazi za wilaya na kata, kuandaa kanuni za uendeshaji, na kushirikiana na Chuo cha Ufugaji Nyuki (BTI) kubadilishana uzoefu. “TABEDO inapaswa kubaki kuwa chombo cha wadau wote wa nyuki na kuhakikisha inafanya vikao kwa mujibu wa Katiba ili kuimarisha uhai wa chama,” alisema Mhe. Pinda.
Vilevile, aliipongeza Bodi kwa uwiano wa kijinsia na umri miongoni mwa wajumbe wake, sambamba na kupongeza mradi wa BEVAC kwa mchango wake katika kuimarisha sekta.
TABEDO imesema itaendelea kuhamasisha wanachama kushiriki maonesho na majukwaa mbalimbali, kufanya kampeni za utunzaji wa mazingira kupitia nyuki, na kusaidia wanachama kupata ufadhili na mitaji ya kuendeleza biashara zao.
0 Comments