Na. Mwandishi Wetu, Dar.
TUZO ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025/2026 ambayo mwaka huu ni msimu wa Nne, tayari Waratibu wa tuzo hizo wametangaza rasmi muda wa kupokea miswada ambayo ni kuanzia Agosti 15 hadi Novemba 30, mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa habari mapema leo Agosti 13, 2025 katika makao makuu ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Mwenyekiti wa Tuzo hiyo, Prof. Penina Mlama amebainisha kuwa Kamati itazingatia masharti na vigezo kwa washiriki wote watakaoshindanishwa.
"Kila Mwandishi bunifu anatakiwa kuzingatia vigezo tulivyoviweka. Hivyo dirisha la kuwasilisha miswada litafunguliwa Agosti 15 hadi November 30, 2025.
Vigezo hivyo vinapatikana katika tovuti ya TET ya (www.tie.go.tz)
“Tumeona tisisitiza waandishi kwamba ni muhimu kufuata vigezo, hata kama kazi ni nzuri kiasi gani kama haijafuata utaratibu haitachukuliwa, sasa ninapata uchungu ninapoona mtu anatumia muda mrefu na akili nyingi kuandika andiko lake zuri alafu anawasilisha linatolewa kwasababu ya kutokufuata utaratibu. Niwasisitize miswada itakayoshindanishwa ni ile iliyozingatia vigezo.
“Tunapokea miswada mingi lakini zaidi ya 40 kila mwaka inawekwa pembezi kwasababu ya kuozingatia vigezo, ni matumaini yangu kwamba waandishi wote watafuata taratibu na vigezo vyote vilivyowekwa, ili zile changamoto zote zilizojitokeza katika awamu zilizopita zisijitokeze, hasa katika matumizi sahihi ya Kiswahili, kutumia Time New Roman, na saizi ziwe 12, na mwanzoni kuwe na ‘double space’,” amesisitiza Prof. Penina.
Ameongeza kuwa washiriki ni lazima wawe watanzania, kazi iwe mpya isichapishwe kokote, mwandishi ataruhusiwa kushiriki nyanja mojawapo kati ushairi, hadithi za watoto, riwaya na Tamthilia, andiko bunifu litakalowasilishwa liwe makini lililojikita katika masuala muhimu ya kijamii.
Ametaja zawadi kwa washindi katika tuzo hizo mshindi wa kwanza atapata Sh. Milioni 10, na kitabu chake kuchapishwa serikali itanunua nakala na kuzisambazwa katika shule zote nchini, wa pili atapata Sh. Milioni saba cheti, na wa tatu Sh. Milioni tano, akisema zawadi hizo ni kwa kila nyanja.
Hata hivyo, alieleza kuwa kutokana na umuhimu wa tuzo hizo kitaifa serikali imewekeza katika kuhakikisha wanafanikiwa kukuza kizazi kipya cha waandishi, kuchochea usomaji na soko la vitabu, kukuza Kiswahili, kuchochea ujifunzaji na kuongeza idadi ya vitabu nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba amesema moja ya majukumu ya taasisi hiyo ni kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mtaala ikiwemo vitabu vya kiada za ziada na kwamba ili kuweza kufanikisha upatikanaji wa vitabu vya ziada wameandaa tuzo hizo kuhamasisha watu kuandika vitabu.
“Tuzo hii inatekelezwa kwa fedha ya serikali na mwaka huu tunatekeleza utoaji wa tuzo kwa mara ya nne, TET tunaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutenga fedha kuhakikisha tuzo hii inaendelea kutekelezwa,” amesema
Amesema baadhi ya malengo ya tuzo hiyo ni kuwatambua kitaifa na kuwazawadia waandishi mahiri wa uandishi bunifu, kukuza lugha ya Kiswahili na utamaduni wa kusoma na kujisomea pamoja na kuongeza hifadhi ya vitabu katika maktaba ya taifa, mikoa, vyuo na shule mbalimbali.
Aidha, Dk Aneth Komba amebainisha kwamba mwaka huu pia washindi watapata fursa ya kutembelea katika vyombo vya habari ili kutangaza kazi zao kwa kina na fursa ya kuelezea ili kutoa elimu kwa wengine namna bora na sahihi ya Uandishi bunifu.
0 Comments