NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
DAR ES SALAAM.Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, imezuiwa kurushwa mubashara au kuchapishwa taarifa za ushahidi baada ya Mahakama kutoa agizo maalum la kulinda mashahidi wa siri wa kiraia.
Akisoma uamuzi huo leo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Franko Kiswaga, amesema zuio hilo limetolewa kwa mujibu wa maelekezo ya Mahakama Kuu. Ameeleza kuwa taarifa za mwenendo wa shauri hilo zitasomewa mahakamani hadharani, lakini utambulisho wa mashahidi wa siri utafichwa.
Hakimu Kiswaga pia ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhariri taarifa za uwasilishaji wa shauri hilo ili kuhakikisha majina na maelezo yanayoweza kumtambulisha shahidi hayatajwe. Ameongeza kuwa mtu yeyote ikiwemo vyombo vya habari atakayetaka kuchapisha taarifa zinazohusu mashahidi atalazimika kupata kibali maalum, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayekiuka.
Katika hatua ya leo, Lissu atasomewa taarifa za mwenendo wa upelekeaji shauri hilo Mahakama Kuu, bila kuhitajika kujibu chochote kwa sasa.
Hata hivyo, nje ya mwenendo wa shauri, viongozi wa Chadema wamelalamikia utaratibu wa ulinzi wa mahakama, wakidai kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliovaa kiraia ndani ya chumba cha mahakama ambao wanaamini ni askari polisi.
Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini ambayo, endapo atatiwa hatiani, adhabu yake ni hukumu ya kifo. Mpaka sasa amekaa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu akisubiri mwenendo wa shauri kupelekwa Mahakama Kuu.
MWISHO.
0 Comments