NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
ZOEZI la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania ubunge limehitimishwa jana Agosti 27, 2025, ambapo vyama viwili kati ya 20 vilivyochukua fomu katika majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo vimeshindwa kurejesha fomu hizo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Vyama vilivyoshindwa kurejesha fomu ni Chama cha Makini (Moshi Vijijini) na NRA (Vunjo), na hivyo kufanya vyama vilivyosalia kuwa 18, ambapo kila jimbo litakuwa na wagombea kutoka vyama tisa.
Shughuli ya uchukuaji wa fomu kwa nafasi za ubunge na udiwani ilianza Agosti 14 na kukamilika jana saa 10 jioni.
Kwa Jimbo la Vunjo, wagombea walioteuliwa wanatoka vyama vya CCM, CHAUMMA, DP, ACT-Wazalendo, ADA-TADEA, MAKINI, CCK, AAFP na TLP.
Miongoni mwa wagombea walioteuliwa ni Enock Koola anayepeperusha bendera ya CCM na Grace Kiwelu kutoka chama cha CHAMA.
Kwa Jimbo la Moshi Vijijini, wagombea walioteuliwa wanatoka vyama vya CCM, CHAUMMA, CUF, CCK, ADA-TADEA, TLP, NRA, ACT-Wazalendo na AAFP.
Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Lucas Msele, alisema jumla ya vyama 10 kwa kila jimbo vilichukua fomu za ubunge, lakini chama kimoja katika kila jimbo kimeshindwa kurejesha.
Mwisho
0 Comments