Header Ads Widget

DR CONGO KUSUSIA MKUTANO WA THABO MBEKI UTAKAOFANYIKA AFRIKA KUSINI

 

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema kuwa itasusia mkutano wa amani uliopangwa kufanyika mnamo mwezi Septemba nchini Afrika Kusini.

Mkutano huo ulioandaliwa na aliyekuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki umewaalika viongozi wa pande zote kwenye mzozo wa DR Congo, pamoja na kundi la waasi la M23 lenye kuungwa mkono na Rwanda.

Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya DRC amesema mkutano huo unaoongozwa na wakfu wa Mbeki haujapangwa kwa muda sahihi na hawajapendezwa nao.

"Tayari tuna njia tatu za kuongoza DRC kufikia amani," alisema Muyaya wakati akidai kwamba taarifa kadhaa za awali za Thabo Mbeki zilionyesha aina ya kutojali ya hali ya sasa ya usalama mashariki ya Congo.

Alisema kuwa DRC inazingatia zaidi mchakato wa amani wa Washington na Doha na vile vile juhudi za pamoja za madhehebu mengi ya kidini huko Congo.

Wajumbe wa serikali na baraza la mawaziri la Rais Félix Tshisekedi walikuwa wamealikwa katika mkutano huo nchini Afrika Kusini.

Bado haijulikani wazi ikiwa M23 itashiriki katika mkutano huo, lakini kiongozi wa harakati za AFC/ M23, Corneille Nangaa alikuwa amealikwa.

Wakfu huo pia ulimwalika Rais wa zamani wa DR Congo, Joseph Kabila na viongozi wengine wakuu wa kisiasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na Moïse Katumbi, Vital Kamerhe, Delly Sesanga, Martin Fayulu, Claudel Lubaya, Seth Kikuni na Jean- Jacques Lumumba.

Mkutano huo umepangwa kufanyika kati ya 3 na 6 Septemba.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI