Header Ads Widget

COOP BENKI NA AGITIF WATOA MKOPO WA BILIONI 8.5 KWA VYAMA USHIRIKA


Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

BENKI ya Ushirika (Coop Benki) kwa kushirikiana na Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo (AGITIF), imetoa mkopo wa shilingi bilioni 8.5 kwa vijana na wanachama wa vyama vya ushirika kutoka maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji mashambani.

Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Benki, Godfrey Ng’urah, alisema mkopo huo utawanufaisha wakulima wote kupitia vyama vya ushirika, 

“Benki ya Ushirika inashirikiana na AGITIF kutoa mikopo kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na vijana na wanawake. Leo tunatoa mkopo wa dhamani ya shilingi bilioni 8.5 kwa dhamira ya kuchochea kilimo chenye tija,” amesema Ng’urah.

Amesema Mfuko wa AGITIF ulianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kutoa huduma za kifedha kwa watu binafsi waliopo katika sekta ya kilimo, taasisi za kifedha na makundi maalum. 

"Mfuko huo umeelekeza nguvu kubwa kwa vijana walio na umri chini ya miaka 40 pamoja na akina mama, " Amesema

Na kuongeza "Hadi sasa, AGITIF imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 94, ambazo zimeelekezwa katika miradi ya umwagiliaji na kuongeza uzalishaji mashambani, " Amesema

Ng’urah amebainisha kuwa Coop Benki itatekeleza jukumu la kuwa wakala wa mikopo hiyo, na kwamba lengo ni kuwafikia wakulima wote walioko maeneo ya vijijini na mijini kupitia mtandao wa vyama vya ushirika na matawi ya benki hiyo kote nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Kilimo,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar amesisitiza kuwa mkopo huo ni wa mzunguko, hivyo ni muhimu urejeshwe kwa wakati.

 “Tunatoa wito kwa wakulima wanaokopeshwa kuhakikisha wanarejesha mikopo hii kwa wakati. Hii itawezesha wengine pia kupata fursa sawa ya kuendeleza shughuli zao za kilimo,” amesema.


Mpango huu unaendana na juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya kilimo kupitia upatikanaji wa mitaji nafuu kwa wakulima, ikiwa ni pamoja na kuboresha tija, kuongeza kipato cha kaya na kuchochea ajira vijijini.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI