Header Ads Widget

WANATAALUMA SUA NA MZUMBE WAIBUA MWELEKEO MPYA WA NISHATI SAFI

 


Na Farida Mangube, Morogoro

Wanataaluma kutoka chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na chuo kikuu Mzumbe wameitaka jamii kuchangamkia matumizi ya nishati safi na jadidifu kama njia ya kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira, sambamba na juhudi za serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui akizungumza katika mkutano wa kitaaluma uliohusisha washirika wa maendeleo kutoka Ulaya na watafiti wa ndani, amesema sasa ni wakati wa kutumia maarifa ya kitaaluma kutengeneza suluhisho la nishati mbadala linaloendana na uhalisia wa Watanzania wa kawaida.



"Sisi kama wanataaluma tunalo jukumu la kutafuta njia bora za kuzalisha nishati mbadala inayoweza kutumiwa kwa urahisi na wananchi vijijini na mijini. Hii inaenda sambamba na kampeni ya Mama Samia inayolenga kutumia nishati safi kama gesi na kuachana na kuni na mkaa," alisema Prof. Hawa


Wanataaluma hao wamesema kuwa tayari wameshirikiana na wenzao kutoka Ulaya kwa kutembelea maeneo ambayo yamefanikiwa kuzalisha nishati mbadala kwa kutumia vyanzo vya ndani kama jua, upepo na mabaki ya mazao.


"Tumejifunza kutoka Ulaya jinsi gani wanaweza kuzalisha nishati katika ngazi ya kijiji, na kuifanya ipatikane kwa watu wote kwa gharama nafuu. Tunaamini njia hizi zinaweza kuleta mageuzi makubwa nchini kwetu kama zikitumika vizuri," aliongeza mtaalamu huyo.


Akizungumza kuhusu hatua za serikali, Prof. Esron Karimuribo, mtafiti kiongozi wa mradi wa Nishati ambaye pia ni Rais wa ndaki ya Tiba ya wanayamana sayansi za afya kutoka Chuo kiuu SUA  amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kupunguza gharama za gesi kwa matumizi ya nyumbani, jambo ambalo limewasaidia wanawake wengi mijini na vijijini kuachana na matumizi ya kuni.



"Mradi huu pia unalenga taasisi zenye watu zaidi ya 100 kama shule na hospitali kuhakikisha zinapata nishati bila kuharibu mazingira. Hili ni jambo kubwa kwa maendeleo endelevu," alisema.

Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imeongeza kasi ya kusambaza nishati safi kupitia ruzuku ya gesi na miradi ya nishati jadidifu, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hasa lengo namba saba linalolenga nishati nafuu na salama kwa wote.

Wanataaluma hao walihitimisha kwa kutoa wito kwa sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na vijana wabunifu kuwekeza kwenye teknolojia rafiki kwa mazingira ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi kwa Watanzania wote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI