Na. Mwaandishi wetu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu ya Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) Abdallah Mfaume amesema kuna kila sababu ya waandishi wa habari kuungana mkono pamoja na kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Mfaume amesema tathmini fupi iliyofanyika inaonesha kuwa kila ifikapo karibu na uchaguzi mkuu waandishi hugawanyika kwa kufata upepo wa vyama vya siasa jambo ni kosa kwa mujibu wa miongozo ya uandishi wa habari.
Mwenyekiti ZAMECO ameeleza hayo katika Mkutano kazi kuhusu tathmini ya miaka mitano kuhusu mchakato wa sheria mpya ya habari kilichojumuisha baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wajumbe kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, ZAMECO pamoja na waandishi wa habari kilichofanyika Ofisi za TAMWA Zanzibar, Tunguu.
Mfaume amesema mchakato wa sheria mpya ya habari unahitaji nguvu za ziada kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kufanikisha marekebisho hayo ambayo yamekuwa kilio cha muda mrefu kwa waandishi wa habari.
Pia amesema, waandishi wengi kwa sasa wamejiingiza katika ushabiki wa kisiasa na baadae baadhi hujigawa kwa kushabikia vyama vya siasa hali inayopelekea kudumaa kwa jitihada za kulitilia mkazo suala la Sheria mpya ya huduma za habari.
"Waandishi wamegawanyika kwa sasa kila mwandishi anashabikia chama chake tena wazi wazi jambo hili halikubaliki na linadumaza harakati za maendeleo kwa wananchi"- alisema Mfaume.
Kupitia kikao hicho, wajumbe wa baraza la wawakilishi wakiwakilishwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said na Mwakilishi wa Jimbo la Pandani, Profesa. Omari Fakih Hamad wamesema wamekuwa mstari wa mbele kuendea mbio marekebisho ya sheria mpya ya habari ambapo mara kadhaa wamekuwa wakihoji hatua iliyofikiwa kwa Serikali.
Wajumbe hao wameipongeza ZAMECO pamoja na TAMWA- Zanzibar kwa juhudi na maarifa katima kuharakisha mchakato wa sheria mpya ya habari iliyoasisiwa toka mwaka 1988.
Awali, Mkurugenzi wa TAMWA- Zanzibar, Dk. Mzuri Issa amesema wamekuwa mstari wa mbele kuwapa elimu waandishi wa habari kwa namna ya kuhamasisha jamii na Serikali kutambua umuhimu wa sheria mpya akitolea mfano kuhusu madhara ya sheria ya sasa katika kuelekea Mchaguzi Mkuu.
Dk. Mzuri amesema sheria ya sasa ya habari, kupitia Sheria ya Tume ya Utangazaji, Sheria ya Uchapishaji wa magazeti na makala, zote zimeonekana kuwa na mapungufu makubwa ambazo haziendani na maisha halisi ya sasa hivyo ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa sheria hiyo ili kusaidia utekekezaji mzuri wa majukumu ya waandishi wa habari.
Zanzibar bado inatumia Sheria ya Huduma za vyombo vya habari ya mwaka 1988 yenye sera ya mwaka 2006 ambapo mpaka sasa ni zaidi ya miaka 20 imepita toka kuanza kwa harakati za mchakato wa sheria mpya ya habari.
0 Comments