Header Ads Widget

UCHAGUZI TANZANIA 2025: KWA NINI IDADI YA WAPIGA KURA TANZANIA 'INAZUA MASWALI'?

 

Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele,

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC) imejikuta katikati ya mjadala baada ya kutangaza kuwa idadi ya wapiga kura katika daftari la kudumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imefikia milioni 37.6.

Takwimu hizi zimezua maswali mazito kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu, wakitaka ufafanuzi wa kina kuhusu uhalali wake, hasa kwa kulinganisha na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Akitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele, alibainisha kuwa kati ya wapiga kura hao, milioni 7.6 ni wapya, sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwemo kwenye daftari mwaka 2020.

Licha ya kuwepo kwa ongezeko la vituo vya kupigia kura vinavyofikia 99,911, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 kutoka vituo 88,567 vya mwaka 2020, mjadala mkubwa umesalia kwenye ongezeko la idadi ya wapiga kura ukilinganisha na watu wenye sifa za kupiga kura kwa mujibu wa Sensa ya 2022, mjadala unaoibua maswali 'tata' matatu.

1. Je, inawezekana nusu ya Watanzania ni wapiga kura?

Kiini cha utata huu kinatokana na kulinganisha idadi hiyo ya wapiga kura na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kwa mujibu wa sensa hiyo, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu milioni 61.7.

Kati ya hao, milioni 30.2 walikuwa na umri wa chini ya miaka 18, hivyo kikatiba hawastahili kupiga kura. Hii inamaanisha kuwa idadi ya watu waliokuwa na umri wa miaka 18 na kuendelea wakati wa sensa ilikuwa takriban milioni 31.4.

Kwa hesabu hiyo, tofauti ya takribani wapiga kura milioni 6.2 kati ya waliotangazwa kuwa kwenye daftari la wapiga kura (milioni 37.6) na wale waliotarajiwa kuwa na sifa ya kupiga kura (milioni 31.4) imeibua maswali. Je, idadi hii ya ziada imetoka wapi?

Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA, John Heche, alihoji kupitia mtandao wa X (zamani Twitter): "Uchaguzi umeshaporwa hata kabla ya siku ya kupiga kura," akidokeza wasiwasi kuhusu takwimu hizo.

Naye Onesmo Olengurumwa kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) alisema: "Nasikia zaidi ya nusu ya Watanzania, milioni 37.6 ni wapiga kura 2025. Kwa sasa tuna watu 70,545,865. Nawakumbusha tu watoto kati ya miaka 0–17 si chini ya asilimia 40 ya population (idadi ya watanzania) kwa mujibu wa sensa."

Martin Maranja, mfuasi wa CHADEMA, alihoji zaidi: "Idadi ya watu 61,741,120 ukitoa idadi ya watoto wa miaka 0–14 ni 26,399,988 unabaki na watu 35,341,132. Haiwezekani wote wakajiandikisha. Watu 2.3M wametoka wapi?"

Swali hili linagusia tofauti ya ndani zaidi ya takwimu halisi na makadirio. Kama watu milioni 35.3 walikuwa watu wazima mwaka 2022, hivyo baadhi ya wanasema inastaajabisha kuona takwimu ya wapiga kura ikikaribia kufikia milioni 37.6 miaka mitatu tu baadaye.

2. Je, takwimu zinakinzana?

Wachambuzi wanaonya kuwa takwimu za sensa na zile za daftari hutofautiana kwa sababu ya malengo, mbinu za ukusanyaji, na uhalisia wa maisha. Kwa mfano, sensa huwalenga watu wote bila kujali umri, lakini daftari huwalenga watu pekee walio na sifa za kupiga kura, ikiwemo umri wa miaka 18 na kuendelea.

Aidha, wapo wanaojiandikisha mara mbili kwa makusudi au kwa nia ya kupata kitambulisho cha mpiga kura kwa matumizi mengine ya kijamii. Wengine hukosa kuhesabiwa wakati wa sensa kutokana na sababu mbalimbali kama uhamaji, mabadiliko ya makazi, au mazingira magumu ya kufikika.

George Semiono, mtaalamu wa takwimu, anasema: "Sio kila mtu mwenye sifa ya kupiga kura anajiandikisha, na sio kila aliyehesabiwa kwenye sensa ni mpiga kura."

Wachambuzi pia wanaonya kuwa idadi ya waliofariki kati ya 2020 hadi 2025 haijaonyeshwa wazi kwenye hesabu ya wapiga kura. Kwa mujibu wa takwimu za World Bank na WHO, Tanzania hupoteza watu zaidi ya 250,000 kila mwaka. Katika kipindi cha miaka mitano, hiyo ni zaidi ya milioni 1.2. Swali linabaki: Je, Tume imeondoa wapiga kura waliopoteza maisha?

Kwa mujibu wa INEC, kulikuwa na wapiga kura 99,744 waliondolewa kwa kupoteza sifa, bila shaka waliofariki pia ni miongoni mwao, wengine 8,703 waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja wakikabidhiwa kwa vyombo vya sheria.

Aidha, kiwango cha ongezeko la watu Tanzania hukadiriwa kuwa kati ya 2.9% hadi 3.2% kwa mwaka. Hii ina maana kuwa kati ya mwaka 2022 na 2025, watu milioni 5.5 hadi 6 wanaweza kuwa wameongezeka. Hii huleta mantiki kuwa watu zaidi ya milioni 67 wanaweza kuwa wapo hadi kufikia uchaguzi wa 2025.

Lakini hata kwa makadirio haya, bado kuna maswali kuhusu msingi wa idadi ya wapiga kura. Semiono anahitimisha kwenye hili kwa kusema: "Ongezeko la daftari linaweza kueleweka kwa wastani wa ukuaji wa watu wa asilimia 3 kila mwaka, lakini hilo haliondoi umuhimu wa uwazi wa takwimu na ukaguzi wa daftari."

Katika kuhakikisha inaondoa mashaka yoyote kuhusu hoja zinazozungumzwa za idadi na masuala mengine muhimu kwenye daftari la kudumua la wapiga kura ikiwemo masuala ya idadi na vituo vya kupigia kura, Tume huru ya Uchaguzi, INEC imewapatia daftari hilo vyama vyote vya siasa.

Alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa Dodoma mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Mwambegele, alisema: "Tarehe 26,Julai, 2025 nilitangaza idadi ya wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na idadi ya vituo vitakavyotumika kupigia kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, napenda kuwafahamisha kuwa leo baada ya kikao hiki nitawapatia nakala ngumu (hard copy) na nakala tepe (soft copy) ya daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na nakala ngumu na nakala tepe ya vituo vya kupigia kura".

Mwenyekiti wa Chama cha wananchi, CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyehudhuria mkutano huo wa Tume na vyama vya siasa, kuhusu mchakato mzima wa daftari la kupiga kura na masuala mengine ya uchaguzi alisifu hatua ya Tume, kuweka wazi daftari hilo kwa vyama vya siasa, ikiwa ni mara ya kwanza vyama kupewa fursa hiyo ili kuweka uwazi na kupunguza malalamiko.

"Jambo ambalo mimi limenipa matumaini sana ni kupewa daftari la wapiga kura, hii haijawahi kutokea, mwaka 2020 hatukukabidhiwa daftari la wapiga kura na (orodha ya) vituo vya kupigia mapema (kama hivi) kuweza kujiandaa, kwa hiyo ni hatua nzuri ukilinganisha na utaratibu ulivyokuwa mwaka 2020", alisema Lipumba.

3. Uchaguzi kuwa huru na haki?

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene

Mashaka haya kuhusu idadi ya wapiga kura yanajengwa juu ya hofu ya kukosekana kwa uchaguzi huru na wa haki. Hii ndiyo maana sheria mpya inasisitiza uwazi.

Kifungu cha 24 (2) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024, pamoja na Kifungu cha 34 cha Kanuni za Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, vinasisitiza kuwekwa wazi kwa daftari la awali kwa ukaguzi wa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi kuhusu uchaguzi huru na haki alitoa hakikisho kwa vyama vyote 19 vya siasa vilivyosajiliwa kikiwemo CHADEMA, ambacho kimetangaza kutoshiriki uchaguzi mpaka kufanyike marekebisho makubwa ya mfumo wa uchaguzi, wanaouona kwa sasa hauko huru na haki.

Lukuvi alisema: "Nataka niwatoe hofu vyama vyote 19 kuwa uchaguzi chini ya Rais Samia utakuwa huru na wa haki."

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha hakuna mashaka kuhusu uchaguzi.

Anazitaja hatua hizo ni Pamoja na kurekebisha sheria za uchaguzi, kuimarisha Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, kutoa elimu ya mpiga kura, kuimarisha usalama na amani, na kuboresha daftari.

Hata hivyo, pamoja na hatua hizi, chama cha Chadema kinasisitiza hakitashiriki uchaguzi, na kupitia kampeni yake ya NO REFORMs NO ELECTIONS, kinaeleza marekebisho na hatua za sasa hayatoi uwanja sawa wa uchaguzi kati ya chama tawala, CCM na vyama vya upinzani.

Uzoefu ukoje kutoka Afrika na nje

Wananchi wa Equatorial Guinea wakipiga kura mwaka 2022

Mjadala wa aina hii si wa Tanzania pekee, hutokea katika nchi nyingi unapofika wakati wa Uchaguzi. Nchini Zimbabwe mwaka 2018, Tume ya Uchaguzi ilitajwa kuruhusu zaidi ya watu milioni 5.8 kupiga kura, wakati sensa ilionyesha watu wazima waliohitimu kupiga kura walikuwa chini ya milioni 5.5.

Mwaka 2016 Equatorial Guinea, wapiga kura walioripotiwa walikuwa 325,548 karibu sawa na watu wote wa umri wa kupiga kura, huku Rais Teodoro Obiang akishinda kwa 92.7%.

Urusi mwaka 2021, baadhi ya majimbo yaliripoti idadi ya wapiga kura iliyozidi idadi ya watu waliopo kwa mujibu wa wachunguzi wa kimataifa.

Halikadhalika, katika nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda, Nigeria, DRC, na Malawi, masuala ya wapiga kura hewa, usajili mara mbili, na majina ya marehemu katika daftari yameibua migogoro mingi. Kwa hivyo, hoja haipo tu kwenye idadi bali kwenye uhalali, usahihi, na uaminifu wa mchakato mzima.

George Semiono anahitimisha kwa kusisitiza kuwa: "Daftari la wapiga kura linapaswa kuwa wazi, kukaguliwa kwa uhuru na kuwa na uwajibikaji wa taasisi ili kulinda misingi ya uchaguzi wa haki." Na kwa msingi huo itapunguza maswali.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI