Nchi 17 zikiwemo Saudi Arabia, Qatar na Misri zimeitaka Hamas kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa unaolenga kufufua suluhu la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina.
Azimio la New York, lililotayarishwa na Ufaransa na Saudi Arabia, waliokuwa mwenyekiti wa mkutano huo, na kuidhinishwa na nchi nyingine 15 (ikiwa ni pamoja na Brazil, Canada, Uturuki, Jordan, Qatar, Misri na Uingereza), pamoja na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu, lilitoa wito wa kusitishwa kwa vita katika Ukanda wa Gaza ili kupata "suluhisho la haki, la amani na la kudumu la mzozo."
Tamko hilo limethibitisha dhamira ya nchi hizo kuchukua hatua madhubuti, za muda na zisizoweza kutenguliwa katika utatuzi wa amani wa suala la Palestina na utekelezaji wa suluhisho la serikali mbili.
Katika muktadha huo, nchi hizo zimesisitiza kuwa, "utawala na udumishaji wa utulivu na usalama katika ardhi zote za Palestina ni lazima liwe jukumu la kipekee la Mamlaka ya Ndani ya Palestina, kwa uungaji mkono ufaao," na kwamba "Israel lazima ijiondoe katika Ukanda wa Gaza... na Hamas inapaswa kukomesha udhibiti wake Gaza na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina."
Wakati huo huo, nchi 17 zilitoa wito wa kupatikana kwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo katika Ukanda wa Gaza, ambao unatishiwa na njaa, na kukataa "matumizi ya njaa kama njia ya vita."
Pia walionesha kuunga mkono "kutumwa kwa ujumbe wa kimataifa wa muda ili kuweka utulivu" huko Gaza.
0 Comments