Header Ads Widget

TUME YA UCHAGUZI YAASISITIZA USIMAMIZI WA RASILIMALI KATIKA UCHAGUZI MKUU




Na Chausiku Said

Matukio Daima - Mwanza

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mara na Mwanza kuhakikisha wanasimamia ipasavyo rasilimali vifaa na fedha katika maandalizi na utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu ujao, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia sheria.

Wito huo umetolewa leo Julai 23, 2025 na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Mjumbe wa Tume hiyo, Asina Omari, wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi kutoka ngazi mbalimbali yaliyofanyika jijini Mwanza.


Jaji Omari alisema ni muhimu kwa wasimamizi hao kuhakiki vifaa vya uchaguzi mara tu wanavyokabidhiwa, na kutoa taarifa mapema iwapo kutakuwa na upungufu, ili kuepusha changamoto wakati wa upigaji kura.

“Ni lazima msimamie vyema vifaa na fedha mtakazotumia kwa shughuli za uchaguzi. Kuweni waadilifu, wenye uwazi na wazingatie maelekezo ya tume,” alisema Jaji Omari.

Aidha, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo ambao ni waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, wasaidizi wa wasimamizi, maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi kuhakikisha wanapeleka elimu waliyoipata kwa watendaji wa kata na vituo vya kupigia kura.

“Pelekeni elimu hii mliyoipata kwa wasimamizi wasaidizi wa kata na watendaji wa vituo kwa weledi ili uchaguzi uwe na ufanisi,” aliongeza.

Mafunzo hayo yaliwalenga kuwajengea uwezo wa kuelewa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI