Header Ads Widget

SOKO LA MASHINE MASHINE TATU IRINGA LATEKETEA KWA MOTO.

 

NA MATUKIO DAIMA APP.

IRINGA.Wafanyabiashara wa Soko la Mashine Tatu, lililoko katikati ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, wamejikuta katika majonzi makubwa baada ya soko hilo kuteketea kwa moto mkubwa usiku wa kuamkia leo Julai 12, 2025..

Moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika rasmi, umeharibu sehemu kubwa ya soko hilo la bidhaa za malimbichi, na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara 515 waliokuwa wakijishughulisha na uuzaji mali mbichi,vitoweo vya kuku,maduka na vibanda katika eneo hilo.

Akizungumza kwa huzuni, mmoja wa wafanyabiashara waliokumbwa na janga hilo Marry Ilomo  alisema, "Tumepoteza kila kitu. Moto umetumaliza. Hatujui pa kuanzia tena." Kauli kama hiyo imetawala miongoni mwa waathirika wengi ambao wamebaki bila msaada, wakiangalia mali zao zikiteketea kwa moshi.

Mashuhuda wanasema moto ulianza majira ya saatano usiku na ulienea kwa kasi kubwa kutokana na kuwepo kwa bidhaa nyingi zinazowaka kwa urahisi, ikiwemo mbao, majani, na plastiki.

Hamisi Kiyemba, mmoja wa wafanyabiashara waliopata athari kubwa katika tukio hilo, ameeleza kwa uchungu jinsi alivyoshuhudia biashara yake ikiteketea mbele ya macho yake, huku akifanikiwa kuokoa vitu vichache sana.

"Nilifika sokoni majira ya saa kumi alfajiri baada ya kupigiwa simu na jirani wangu, Nilipofika, kila kitu kilikuwa tayari kimeanza kuungua. Nilijitahidi kuingia kwenye kibanda changu na kuokoa baadhi ya makaratasi na mizigo michache ya thamani, lakini sehemu kubwa ya bidhaa zangu za biashara zimeteketea," alisema Kiyemba


Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Iringa,Benjamini Sitta, baada ya kutembelea eneo la soko la Mashine Tatu lililoteketea kwa moto na kuwapa pole wafanyabiashara waliopoteza mali zao huku akiwahakikishia kuwa serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema hatua za haraka zinaendelea kuchukuliwa ili kusaidia kurejesha mazingira ya kufanya biashara, huku akisisitiza kuwa serikali haitawaacha peke yao.

"Ninawaomba muwe na subira, Serikali inatambua umuhimu wa soko hili kwa maisha yenu na uchumi wa wilaya yetu. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha mnarejea kwenye shughuli zenu mapema iwezekanavyo,"

DC Sitta alikagua athari zilizosababishwa na janga hilo na na kusema kuwa wanashukuru mpaka kufikia muda huu moto umeweza kutulizwa huku meza zote zikiwa zimeteketea.

"Kwa sasa tunaendelea kufanya tathimini ili kuweza kuona ni madhara na wangapi wameathilika ili kuona namna gani tunaweza kushirikiana nao katika kuwatafutia eneo lingine,Mpaka sasa tathimini inaendelea kuna maafisa biashara,katibu wa soko,kikosi cha zimamoto na wengine wakiendelea kufanya tathimini ya madhara yaliyofanyika"

"Eneo hili ni eneo la BAKWATA sio eneo la serikali kwa maana ya halmashauri tunashirikiana nao kuhakikisha kila jambo linarudi katika hali yake"

Mkuu wa Wilaya alisema kuwa Halmashauri itaona namna ya kuweza kuwasaidia wale walioathirika zaidi katika ajali hiyo ya moto kwa kuwa wengi wao mali zao zote zimeteketea.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Iringa Kabigili Said amesema kuwa wamepata taarifa saa 8 usiku ambapo moto ulikuwa umeshika kasi huku vyombo vya usalama na uokoaji vikifanya jitihada kuzima moto huo.

Alisema kuwa katika soko hilo takribani meza 429, maduka ya nje 86, ambayo jumla yake ni wafanyabiashara 515 ambao wameathirika kwa kupoteza mali zao katika soko hilo baada ya moto kuzuka.

"Ninawaomba wafanyabiashara wasitafute mchawi  hali imetokea ni janga Mungu ndio anamipango yake wala sisi tusitafute mahala pa kwenda kuangukia, ni jukumu letu sasa BAKWATA kuhakikisha jambo hili linakuwa la muda mfupi kwa kushirikiana na serikali ili kurejesha hali ya awali"alisema 

Kiongozi wa wafanyabiashara wadogo katika soko hilo Yahya Mpelebwa alisema kuwa wafanyabiashara wengi wamepoteza mali zao ambao walikuwa wamewekeza tofauti tofauti, huku wengine wakiwa na mitaji binafsi na wengine walikopeshwa.

Mpelebwa alisema kuwa wanaiomba serikali, watu binafsi na taasisi za mikopo ambazo wafanyabiashara hao walikopa kuweza kuwavumilia kwa muda mpaka pale hali itakapokaa sawa.

"Rai yetu kama wanairinga tunaomba serikali iweze kuwapatia mbadala wa haraka wafanyabiashara hao waweze kurudi katika biashara zao, kwa kuwa katika kipindi hiki watalazimika kufanya marejesho kwa waliokopa na kufanya maisha mengine yaendelee"

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Jackline Mtei, amesema kuwa walipokea taarifa kwa haraka na kufika eneo la tukio kwa muda, wakifanikiwa kuzuia moto usienee zaidi.

"Moto ulikuwa mkubwa sana,tumefanikiwa kuuzima kwa kushirikiana na wananchi, lakini uharibifu tayari ulikuwa mkubwa."

Mpaka sasa, mamlaka za serikali na manispaa zinaendelea na tathmini ya uharibifu ili kujua kiasi halisi cha hasara, huku wito ukitolewa kwa wamiliki wa biashara kuwekeza katika vifaa vya tahadhari ya moto.

MWISHO.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI