William Ruto wa Kenya aliingia madarakani kwa kujenga matumaini makubwa miongoni mwa watu wa kawaida ambao walitarajia angetimiza ahadi zake za kuboresha maisha yao. Badala yake, anakabiliwa na ukosoaji usiokoma - unaoonekana kuwa mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Akionekana kukasirishwa na nguvu ya upinzani, aliuliza Jumatano wiki hii kwa nini hasira kama hiyo ya umma haikuwahi kuelekezwa kwa watangulizi wake, akiwemo Daniel arap Moi, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miongo miwili iliyoadhimishwa na ukandamizaji wa kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu, na wengine walioondoka baada ya uongozi wao kukumbwa na masuala utata.
Jumatano Julai 9, Ruto aliuliza: "Machafuko haya yote, kwa nini hayakuelekezwa kwa (marais wa zamani) Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta…Kwa nini kuna dharau na kiburi?"
Wachambuzi wanaelezea wimbi la sasa la hasira ya umma dhidi ya Rais Ruto, ambalo limeshuhudia zaidi ya watu 100 wakiuawa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kuwa "lisilo na kifani", na kuwaunganisha Wakenya katika migawanyiko ya kikabila, kidini na kitabaka.
Maandamano dhidi ya utawala wake yalianza mwaka mmoja tu baada ya kuingia madarakani. Miaka mitatu baadaye, Wakenya wengi waliokasirika sasa wanataka aondoke - huku kukiwa na maandamano yasiyoisha na wito wa "Ruto lazima aondoke" na "Ruto Wantam" (Ruto kwa muhula mmoja).
Ruto alipokuwa akiwania urais, alijidhihirisha kuwa mtu wa kawaida, aliyetoka katika maisha ya utotoni yenye umaskini na ustahimilivu. Alitoa wito kwa watu wa kawaida kama mtu ambaye wanaweza kupata msukumo kutoka kwake - baada ya kuinuka kutoka kuwa muuza kuku hadi rais.
Tofauti na hali hiyo na mwanzoni mwa mwaka huu, wakati gazeti moja lilipoandika kichwa cha habari kikiuliza ikiwa Ruto alikuwa "rais anayechukiwa zaidi wa Kenya", hisia ambayo mara nyingi imekuwa ikijitokeza kwenye mitandao ya kijamii na mijadala ya umma.
Inaashiria mabadiliko ya ajabu katika siasa za Kenya, mara nyingi huchangiwa na uaminifu wa kikabila na migawanyiko ya kitabaka. Jinsi Ruto alivyoonekana kuvuka vizuizi hivyo ili kunyakua urais, mienendo hiyo hiyo sasa inaonekana kuwa dhidi yake.
Juma hili msemo "Sisi sote ni Wakikuyu," ulivuma kwenye mitandao ya kijamii huku vijana wakikataa majaribio ya kurejesha migawanyiko ya kikabila ambayo imekuwa ikizikumba siasa za Kenya kwa muda mrefu. Simulizi ya kupingana na "Sisi sote ni Wakenya" iliibuka lakini haikufaulu kupata mvuto sawa - huku wengine wakiiona kama jaribio la kufifisha usemi wa mshikamano katika ujumbe wa kwanza.
Wakikuyu, kabila kubwa zaidi nchini Kenya kutoka eneo la Mlima Kenya, walimuunga mkono kwa kiasi kikubwa Ruto katika uchaguzi wa 2022, pamoja na Rigathi Gachagua, anayetoka eneo hilo, kuwa naibu wake.
Lakini hatua ya kumuondoa Gachagua ofisini mwaka jana kupitia mchakato mkali wa kuondolewa madarakani, ambao aliutaja kama usaliti, ulizua kutoridhika katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wanasiasa wanaoegemea upande wa Ruto wamewashutumu Wakikuyu kwa kuchochea upinzani dhidi ya rais.
Mchambuzi wa kisiasa Mark Bichachi anasema upinzani dhidi ya rais hausukumwi kikabila, lakini unafanyika katika jamii mbalimbali mijini na vijijini.
Anataja "malalamiko ya umma dhidi ya rais na serikali" "isiyo na kifani" na "kihistoria", hata kupita misukosuko ya kisiasa ya miaka ya 1980 na 1990 wakati Moi alipoiongoza serikali ya chama kimoja.
Kipindi hicho kilikuwa na dhuluma za kikatili na vita vya umwagaji damu vya demokrasia ya vyama vingi, lakini Bw Bichachi alisema kwamba hali hiyo haikusababisha shinikizo kama la sasa linalomkabili Rais Ruto, akiongeza kuwa mivutano hiyo ilihusishwa na Vita Baridi na ilionekana kote barani Afrika.
0 Comments