Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma
MKOA wa Shinyanga umefanikiwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda na biashara ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatua iliyochangia ongezeko la uzalishaji, fursa za ajira, na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 14 , 2025 kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM na mafanikio ya serikali mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, jambo lililowezesha kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Amesema moja ya mafanikio makubwa ni kuanzishwa kwa Kongani Maalumu ya Uwekezaji ya Buzwagi (SEZ), ambapo hadi sasa kampuni ya East Africa Conveyers Service imeanza rasmi uzalishaji, huku kampuni nyingine nne zikiwa katika hatua za kupata leseni na kufanya usajili wa mazingira kupitia NEMC ambapo kampuni 15 zaidi zimeonyesha nia ya kuwekeza katika kongani hiyo.
Katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, idadi ya viwanda vikubwa imeongezeka kutoka 36 hadi 40, wakati viwanda vya kati vimeongezeka kutoka 180 hadi 192 na viwanda vidogo kutoka 999 hadi 1,225, ongezeko linalodhihirisha mafanikio ya mpango wa viwanda kwa mikoa.
Mhita amesema kuwa kongani nyingine zimeanzishwa na kuendelezwa katika maeneo ya Nyashishi, Busoka na Buzwagi, sambamba na ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao, ambalo linalenga kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Kupitia sekta hii ya viwanda, Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kutoa jumla ya ajira 50,000, ambapo ajira za muda ni 35,000 na ajira za kudumu ni 15,000 katika kipindi hicho.
"Mafanikio haya ni matokeo ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhamasisha uwekezaji, kuboresha miundombinu na kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi," Amesma Mkuu huyo
Mhita ameongeza kuwa serikali ya mkoa itaendelea kuwahamasisha wawekezaji zaidi na kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha viwanda vinakuwa chachu ya maendeleo ya watu na kuongeza pato la taifa kupitia mnyororo wa thamani wa bidhaa mbalimbali.
Mwisho
0 Comments