NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
MKUU wa mkoa wa Iringa Kheri James amesema wilaya ya Iringa vijijini ni wilaya yenye miradi mingi ya kimkakati ambayo Rais Dkt Samia amedhamilia kuona uchumi wananchi na wilaya hiyo unakua huku akiagiza stendi zote kuanza kazi ndani ya miezi miwili kuanzia leo.
kuwa miradi ya umwagiliaji Pawaga ambao unagharimu zaidi ya Bilioni 5 ,mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa -Hifadhi ya Ruaha ni miradi mikubwa ya kimkakati ukiacha miradi ya umeme,maji na afya inayoendelea.
Hivyo aliwataka watumishi wa Halmashauri hiyo kusimamia skimu ya umwagiliaji Pawaga na miradi mingine ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo .
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini leo wakati wa ziara yake ya kujitambulisha toka alipoteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka mkuu wa wilaya ya Iringa na kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa.
Alisema kwa upande wake amekuwa mkuu wa wilaya ya Iringa na siku zote alifanya kazi ya kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi na ataendelea kufanya hivyo kwa nafasi ya ukuu wa mkoa .
Alisema angetamani kuona watumishi wanasaidia ustawi wa wananchi katika maendekeo yao kwa watumishi wa wa umma kusimamia vema makusanyo ya mapato na kuyawekea bajeti .
"Ni wajibu wenu Halmashauri kushirikiana na TARURA na idara nyingine kusimamia miradi na kuhakikisha fedha zote zinapita kwenye mifumo halisi badala ya kuruhusu fedha mbichi kupewa nafasi kwa watu ama mtu mmoja mmoja kukusanya pesa taslimu na kuweka mfukoni mwake"
Kuwa kufanya hivyo ni kuikosesha serikali mapato na kuifanya Halmashauri kuendelea kushindwa kutekeleza malengo yake.
Mkuu huyo wa mkoa alisema Halmashauri ya Iringa ina pesa nyingi zinazotokana na utalii,kilimo,ufugaji na miradi mingine mingi inayosababisha mapato kukuwa na kuwa jukumu la watumishi ni kusimamia mapato.
Alisema vyanzo vya mapato ni vema kusimamiwa vizuri na kama chanzo cha mapato ni kilimo cha ufuta basi kuongeza nguvu zaidi katika kilimo hicho kwa kupeleka maofisa ugani ili kutoa elimu zaidi kwa wakulima waweze kuzalisha kwa wingi zao la ufuta.
Katika Hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa alisema anashangazwa kuona Halmashauri hiyo kukosa mradi wa stendi wakati kupitia mradi huo ungeweza kuongeza mapato .
Hivyo kuiagiza Halmashauri hiyo kuhakikisha maeneo yote yaloyotengwa kwa ajili ya miradi ya stendi ndani ya miezi miwili stendi zote zinaanza kufanya kazi .
"Halashauri ya Iringa vijijini pekee ndani ya mkoa huo ndio isiyo na stendi yake jambo ambalo haliwezekani lazima Halmashauri hiyo kubadilika haraka "
Kuwa suala la stendi halina siasa kwa sasa kwani kama madiwani walikuwa wakileta siasa kwa sasa hawapo na pindi watakaporejea watakuwa miradi yote ya stendi inafanya kazi.
Kheri alisema Halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini inayo nafasi kubwa ya kuipanga vema wilaya hiyo kiuchumi na kuwa na uchumi mkubwa zaidi .
"Haiwezekani mtu anayefuga wanyama akawa na mapato makubwa kuliko wewe mwenye hifadhi kwani Halmashauri hiyo haipaswi kuwa nyuma kiuchumi wakati wanayo hifadhi kubwa ya Ruaha ambayo wakiitumia vizuri ni utajiri mkubwa"
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alisema kauli mbiu ya mkoa wa Iringa ni "IRINGA IMARA TUTAIJENGA KWA UMOJA NA UWAJIBIKAJI"kuwa kauli mbiu hiyo haitafanya kazi kama watumishi hawatakuwa wabunifu ni watumishi waoga katika kushauri mambo .
0 Comments