Header Ads Widget

MARA YANUFAIKA NA MAGEUZI CHANYA YA MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA KANALI MTAMBI

 

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema kuwa mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza leo Julai 18, 2025 na waandishi wa habari, Kanali Mtambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeleta mageuzi yanayoonekana katika sekta ya uvuvi, elimu, afya, miundombinu, na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

“Katika kipindi hiki kifupi cha miaka minne, tumeshuhudia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo imegusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan vijana na wanawake,” alisema Kanali Mtambi.

Alieleza kuwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Serikali imetoa mikopo kwa vikundi na wananchi binafsi kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria. 

Amesema Hadi Juni 30, 2025, mkoa ulikuwa na wafugaji 39 wa samaki kwa vizimba, wakimiliki jumla ya vizimba 241.

Aidha, jumla ya wanufaika 20 kutoka wilaya za Rorya, Bunda na Musoma wamepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,227,350,000, ambayo imewawezesha kumiliki vizimba 9 na boti 11, ikiwa ni hatua ya kukuza ajira na uchumi wa wananchi wanaozunguka Ziwa Victoria.

Katika sekta ya elimu na afya, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali imejenga na kukarabati shule na vituo vya afya katika maeneo ya vijijini, sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau wa maendeleo.

 “Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuamini na kutupatia rasilimali za kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli ambapo Wananchi wa Mara sasa wanaiona Serikali kwa vitendo,” aliongeza Kanali Mtambi.

Amesema pia kuwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeendelea kuimarika katika halmashauri za mkoa huo, hatua inayochochea ushiriki wa makundi hayo katika uchumi wa Taifa.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI