Watumishi wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro wamepongezwa kwa utendaji kazi wao na bidii iliyoiwezesha Mamlaka hiyo kufikia malengo iliyojiwekea kati mwaka wa Fedha 2025/25.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro NCAA, Bw. Abdul-razaq Badru ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa NCAA Wilayani Karatu Mkoani Arusha ambapo alieleza kuwa katika Mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka hiyo ilijiwekea lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 230 lakini ikavuka lengo hilo na kukusanya shilingi Bilioni 269.9.
Aidha amesema mapato yaliyokusanywa kutokana na shughuli za utalii ni Bilioni 262.74, mapato ya Pori la akiba Pololeti shilingi Bilioni 3.7 na mapato yaliyokusanywa kwenye vyanzo vingine vya mamlaka hiyo yakiwa Shilingi Bilioni 3.274 na kuongeza kuwa wageni wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro wameongezeka kutoka wageni 908,000 mwaka 2023/2024 hadi kufikia wageni 1,061,620 mwaka wa fedha 2024/2025.
Badru amewashukuru pia watumishi hao kwa kuhamasisha upigiaji kura wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika kinyang’anyiro cha World travel awards na kuiwezesha hifadhi hiyo kutangazwa kuwa kivutio bora cha utalii Afrika mwaka (Africa’s leading tourist attractions 2025) katika tuzo zilizotolewa tarehe 28 Juni, 2025.
Amebainisha kuwa kwa sasa Mamlaka hiyo inaandaa mkakati wa miaka mitano ijayo ambapo mkakati huo utashirikisha kila mtumishi kujiwekea shabaha, malengo yanayopimika katika utendaji kazi na kubainisha kuwa mkakati huo pia utaendana na dira kuu ya taifa ya mwaka 2050 ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
0 Comments