Header Ads Widget

MTUHUMIWA WA WIZI WA VIFAA VYA TANESCO AFARIKI DUNIA BAADA YA KUKAMATWA

 

NA CHAUSIKU SAID 

Matukio Daima Mwanza. 

Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu wa jinsia ya kiume kwa tuhuma za kuiba vifaa vya umeme katika karakana ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyopo mtaa wa Isengeng’he, Kata ya Mhandu, Wilaya ya Nyamagana, huku mtuhumiwa mmoja akifariki dunia baada ya kujeruhiwa wakati wa tukio hilo.

Tukio hilo limetokea usiku ambapo watu hao walinaswa na walinzi wakiwa wanapakia vipuli vya umeme aina ya Polymeric na reflector jaketi tatu kwenye gari aina ya Toyota Wish lenye namba za usajili T.285 BWA rangi nyeusi.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Willibroad Mutafungwa, amesema kuwa walinzi wa karakana hiyo walibaini tukio hilo la wizi na kufyatua risasi hewani kwa kutumia bunduki aina ya shot gun, jambo lililosababisha watuhumiwa kutawanyika.

"Baada ya risasi kusikika, askari waliokuwa doria walifika kwa haraka eneo la tukio na kushirikiana na walinzi kuwakamata watuhumiwa waliokuwa bado katika eneo hilo,” alisema Kamanda Mutafungwa.


Watuhumiwa waliokamatwa wametajwa kuwa ni Venister Mladi (24) mkulima na mkazi wa Nyegezi, Yusuph Bilamata (25) fundi aluminium mkazi wa Usagara, Wilaya ya Misungwi, na Lugaila Ibrahimu (24) dereva wa teksi mkazi wa Kishiri, ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari lililotumika.

Kamanda Mutafungwa aliongeza kuwa mmoja wa watuhumiwa alijeruhiwa kichwani sehemu za utosini baada ya kuangukia vyuma vilivyokuwa kwenye karakana hiyo wakati akijaribu kukimbia ili asikamatwe.

"Watuhumiwa wawili walipelekwa Kituo cha Polisi Nyakato kwa hatua zaidi za kisheria, huku majeruhi akipelekwa katika Hospitali ya Sekou-Touré kwa matibabu, lakini alifariki dunia majira ya saa 5 asubuhi,” alieleza Kamanda huyo.


Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku likitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana nalo katika kutoa taarifa za uhalifu kwa ajili ya kuimarisha usalama katika jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI