Na Matukio Daima Media
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), imefanikiwa kutoa mikopo ya shilingi trilioni 1.129 kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa miaka kumi tangu kuanzishwa kwake ambapo wanufaika wamefikia 1,953,162.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Frank Nyabundege wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu benki hiyo kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na ushiriki wa benki hiyo kwenye maonyesho ya nane nane jijini Dodoma.
Alisema asilimia 77 ya mikopo hiyo imetolewa kwenye miaka minne ya utawala wa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba benki hiyo ya kimkakati imekuwa ikiwezeshwa ili kuongeza upatikanaji wa chakula na kuongeza mikopo kwenye sekta ya kilimo.
Alisema benki hiyo tangu mwaka 2018 imekuwa ikitoa dhamana kwa taasisi mbalimbali za fedha ili ziweze kuwakopesha wakulima wadogo wadogo baada ya tafiti kuonyesha kuwa hawakopesheki kutokana na kukosa dhamana za kukopa.
Alisema tangu aingie madarakani Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuboresha kilimo ambapo wakati anaingia madarakani mwaka 2021 alikuta bajeti ya sekta ya kilimo ikiwa shilingi bilioni 294 lakini kwenye utawala wake imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia trilioni 1.2.
“Serikali iliamua kuanzisha benki hii kama mkakati wa kuinua sekta ya kilimo baada ya kuona wakulima wengi hawakopesheki kwa hiyo mikopo hii imesaidia sana kuinua sekta ya kilimo kwasababu wakulima kupitia TADB wanapata mtaji wa kutosha, wanalima kisasa na wanarejesha mikopo yao kwa wakati,” alisema
Alisema mwaka 2018 serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (Small Holders Farmers Credit Guarantee Scheme - SGS) ambao umewanufaisha wananchi 762,291 kwa kutoa mikopo yenye jumla ya shilingi billion 447.95.
Mkurugenzi alisema benki hiyo ilikuwa ikikopesha wastani wa shilingi bilioni 20 kwa mwaka lakini tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021 mikopo inayotolewa na benki hiyo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Alisema mwaka 2021 Rais Samia alipoingia madarakani mikopo hiyo iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 21, mwaka 2022 iliongezeka hadi bilioni 75, mwaka 2023 ilifikia shilingi bilioni 250 na mwaka 2024 ikafikia bilioni 381.
“Wakati Rais Samia anaingia madarakani TADB ilikuwa benki ndogo sana (benki ya hadhi ya daraja la tatu) lakini ndani ya muda mfupi imekuwa kutoka benki ndogo hadi kuwa benki kubwa (benki ya daraja la kwanza), Rais Samia aliingia madarakani, TADB ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni 60 lakini kwa miaka minne aliyokaa madarakani ametupa mtaji na sada mtaji wa benki ni bilioni 442,” alisema
Alisema mbali na Rais kutoa mtaji kwa benki hiyo lakini kwa muda wote amekuwa akiitafutia washirika wa nje ya nchi ambao wamekuwa wakiisaidia kwa mikopo ya masharti nafuu akitoa mfano wa ziara yake ya Ufaransa ambayo ilisababisha benki hiyo ipate mkopo wa shilingi bilioni 210.
Alisema mwaka jana shirika la JICA liliipatia TADB mkopo wa shilingi bilioni 354 fedha ambazo alisema zimeifanya benki hiyo kuwa na nguvu kubwa ya kuendelea kukopesha wakulima kwenye mikoa mbalimbali.
Mkurugenzi alisema kutonana na mafanikio waliyoyapata ndani ya muda mfupi kumekuwa na msururu wa taasisi za fedha kutoka kwenye mataifa mbalimbali ambao wamekuwa wakija kujifunza namna TADB ilivyofanikiwa kuwafikia wananchi wengi kwa mikopo ya kilimo.
0 Comments