NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) Grace Victor Tendega, ameishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kalenga kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Akizungumza na Matukio Daima Media leo mara baada ya kutangazwa kwa jina lake miongoni mwa walioteuliwa kuwania nafasi hiyo, Tendega alisema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake binafsi na ameupokea kwa moyo wa shukrani na kujituma kwa ajili ya kuliletea maendeleo jimbo hilo muhimu katika mkoa wa Iringa.
“Ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa kielelezo cha uongozi bora na kuniamini kuwa miongoni mwa wale wanaopaswa kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi ujao,” alisema Tendega.
Aidha, aliipongeza Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iringa Vijijini inayoongozwa na Mwenyekiti wake Costandino Kihwele pamoja na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa chini ya Mwenyekiti Daud Yassin kwa kuonyesha imani kubwa kwake na kupendekeza jina lake katika mchakato wa uteuzi.
“Nawashukuru kwa mapendekezo yenu na kuonyesha imani kubwa kwangu. Ni jambo linalotia moyo na kunifanya nione wajibu mkubwa wa kuwatumikia wananchi wa Kalenga kwa bidii na uadilifu,” alisisitiza.
Tendega alisema iwapo atapitishwa rasmi kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa 2025 na hatimaye kuchaguliwa na wananchi, ataweka kipaumbele katika kuwaletea maendeleo endelevu wakazi wa jimbo hilo kwa kushirikiana nao kwa karibu.
“Naahidi kuwa nitatenda haki kwa nafasi hii kwa kufanya kazi bega kwa bega na wananchi. Nitajikita katika kusikiliza kero zao na kutafuta majibu kupitia utekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo,” aliongeza.
Tendega, ambaye aliwahi kuwania nafasi hiyo ya ubunge kwa tiketi ya vyama vya upinzani – kwanza kupitia Jahazi Asilia na baadaye CHADEMA – alisema anaifahamu vyema Kalenga, watu wake na changamoto zao, hivyo hahitaji utambulisho mpya katika eneo hilo.
“Kwa vipindi viwili tofauti niligombea ubunge Kalenga, najua vizuri mazingira ya jimbo hili, mahitaji ya wakazi wake na matarajio yao. Nimewahi kushirikiana na wananchi wa makundi yote – ndani na nje ya CCM – na naamini uzoefu huo utanisaidia kuwa mwakilishi bora,” alisema.
Alisema dhamira yake kuu ni kuhakikisha Kalenga inapiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia ushirikiano wa dhati kati ya wananchi, viongozi wa chama na serikali, na utekelezaji wa ilani ya CCM kwa ufanisi mkubwa.
Aliongeza kuwa hatakubali kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi, bali atakuwa daraja la kuunganisha juhudi za viongozi na wananchi ili kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote wa Kalenga.
Kwa sasa, Tendega anajiandaa kuanza kampeni za ndani za chama ikiwa ni sehemu ya kuelekea uteuzi wa mwisho wa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, huku akiendelea kujenga matumaini miongoni mwa wana CCM kuwa atakuwa chaguo sahihi kwa Kalenga.
Jimbo hilo la Kalenga wangine walioteuliwa na kutangazwa na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Taifa ni pamoja na Grace Tendega ni Jackson Kiswaga,Mussa Leonard Mdede,SPA. Henry Nyaulingo
0 Comments