Na Fatma Ally Matukio na Habari
Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika banda la Shirika la Uwakala wa meli Tanzania (TASAC) ili kuweza kupata fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya usafirishaji wa majini.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mohamed Salum wakati alipotembelea banda hilo lililopo katika maonyesho ya 49 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba.
Amesema kuwa, sekta ya usafiri majini inauhaba mkubwa wa mabaharia hivyo, ni vyema wananchi kufika katika banda hilo ili kupata maelekezo ya namna ya kujiunga katika chuo cha ubaharia DMI ili kuweza kupata fursa hizo.
"Takwimu za dunia zinaonesha kuna uhaba mkubwa wa watumishi katika sekta ya bahari licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na pato la taifa"
Ameongeza"Sekta hii kibiashara duniani, inachangia asilimia 90 ya mizigo inayotoka nchi moja kwenda nyengine, hivyo ni vyema wananchi wakapata elimu juu ya sekta ya usafirishaji"amesema
Amesema kuwa, miongoni mwa majukumu ya TASAC ni kudhibiti shughuli za usafirishaji majini ikiwemo kuvisajili vyombo vinavyojengwa nchini na kuvikagua kila hatua na kuvipa vyeti vya ubora pia wanakagua meli za kimataifa zinazoingia nchini.
"Pia tunadhibiti na kutoa na kutoa leseni za bahari, tunasimamia bandari kavu, ndio maana tupo hapa kwa ajili ya kuwahabarisha wananchi waelewe mchango wa TASAC katika kukuza pato la taifa hasa kwenye shughuli za usafirishaji"
Ameongeza kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kuelewa TASAC wanafanya nini kwani licha ya kusimamia shughuli za usafirishaji majini lakini pia kuna fursa nyingi katika sekta hiyo.
"Wataalam mbalimbali waliopo katika banda letu watawaelezea majukumu yanayofanywa na fursa zinazopatikana sekta ya usafirishaji kwani kuna mafunzo ya kitaalam ambayo hayana watu, ukifika hapa wataalam watakuelezea ajira zipo "amesema Salum.
0 Comments