Header Ads Widget

BODI YA NYAMA YAWATAKA WADAU KUHUWISHA VIBALI VYAO KABLA YA MWISHO WA JULAI


NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imewataka wadau wote walioko kwenye mnyororo wa thamani ya nyama kuhakikisha wanahuisha vibali vyao ndani ya mwezi Julai ili kuepuka tozo na adhabu zitakazotolewa baada ya muda huo kumalizika.

Kauli hiyo imetolewa na Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Ziwa, Nemesius Charles,  na kueleza kuwa uhuishaji wa vibali ni sehemu ya mpango wa serikali wa kurasimisha sekta ya mifugo ili kuhakikisha wadau wanatambulika rasmi na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali na taasisi za kifedha.

“Kupitia taasisi ya Bodi ya Nyama, tumekuwa tukiwasajili na kuwarasimisha wadau ili kuhakikisha kuwa shughuli zao zinatambulika kisheria. Kupitia urasimishaji huu, wamefunguliwa fursa mbalimbali, zikiwemo mikopo kutoka benki na taasisi nyingine za fedha,” alisema Charles.

Charles alieleza kuwa serikali inalenga kuhakikisha sekta ya mifugo inachangia ipasavyo katika kukuza uchumi wa taifa, kwa kuhimiza ufugaji wa kisasa na unaozingatia kanuni bora za uzalishaji wa nyama.

“Serikali yetu inapambana kuhakikisha kuwa tunakuwa na ufugaji bora. Sio bora tu kufuga, bali tunalenga wadau wafuge kisasa, kwa tija, na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, ili waweze kuongeza kipato na kukuza biashara zao,” alisema Charles.

Katika kipindi hiki cha mwezi Julai, Bodi ya Nyama inaendelea na ukaguzi kwa wadau wote wa sekta ya nyama katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, kwa lengo la kuhakikisha kwamba kila mmoja anazingatia sheria na kanuni za sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa na vibali halali.

“Kwa sasa sisi kama taasisi tunashughulika na kuhuwisha kazi za wadau kupitia ukaguzi unaoendelea. Tunataka kuhakikisha kuwa kila mdau aliye kwenye biashara ya nyama anakuwa na vibali vinavyotambulika,” aliongeza.

Aidha Charles akifafanua kuwa wadau wametakiwa kutumia mfumo wa MIMIS kwa ajili ya kuhuisha vibali vyao kwa mujibu wa taarifa ya Bodi hiyo, kipindi hiki cha Julai kinatumika kama fursa ya kuhuisha vibali kwa hiari bila adhabu yoyote. Hata hivyo, baada ya kipindi hicho kupita, hatua ya uhuishaji italazimisha kulipa faini kwa mujibu wa sheria.

“Kwa kipindi hiki cha mwezi wa saba, wadau wanaruhusiwa kuhuisha vibali vyao kwa hiari bila adhabu. Lakini baada ya muda huo kupita, watahuisha kwa kulipia faini,” alifafanua Charles.

Bodi ya Nyama Tanzania imetoa wito kwa wadau wote wa sekta ya nyama wakiwemo wafugaji, wachinjaji, wasambazaji, na wauzaji wa bidhaa za nyama, kuwasiliana na wataalamu wa ofisi za Bodi au kuingia kwenye mfumo wa MIMIS, ili kuhakikisha wanatimiza masharti ya kisheria kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI