Header Ads Widget

WAZIRI SIMBACHAWENE ;MIFUMO YA KIDIGITALI YALETA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA UMMA

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodoma

WAZIRI 1wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanachochea ukuaji wa utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na itikadi chanya ya utumishi kwa umma nchini.

Akizungumza jijini Dodoma baada ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali za serikali yanayoshiriki katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Waziri Simbachawene alisema kuwa taasisi nyingi zimepiga hatua kubwa katika kujenga mifumo ya kidijitali, hatua inayowezesha utoaji wa huduma kwa haraka, kwa ufanisi na kwa uwazi zaidi.

“Mabanda niliyotembelea yote yameonyesha maendeleo makubwa ya kidijitali. Mifumo hii inawasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi, jambo ambalo linakwenda sambamba na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha utoaji wa huduma kupitia TEHAMA,” alisema Simbachawene.

Alizipongeza taasisi zote 185 zilizoshiriki kwenye maonesho hayo, akizihimiza taasisi ambazo bado hazijajiunga na mifumo ya kidijitali kufuata mkondo huo kwa haraka.

“Hongereni kwa taasisi zote 185 mlizoshiriki. Kwa zile ambazo bado, zifanye jitihada za kuunganishwa na mifumo hii kwa kuwa imeleta mageuzi makubwa katika utendaji kazi wa serikali,” aliongeza.

Aidha, Waziri Simbachawene alisisitiza kuwa taasisi zote za serikali zinapaswa kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa haraka na kwa gharama nafuu. Alitoa wito kwa wananchi kufika katika viwanja vya maonesho vilivyopo Dodoma kupata huduma mbalimbali moja kwa moja kutoka kwa taasisi za serikali.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu – Utumishi, Juma Nkomi amesema  maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 15 hadi 23 Juni, ambapo kilele chake huadhimishwa rasmi Juni 23.

Amesema Tangu kuanza kwa wiki hiyo, taasisi mbalimbali za serikali pamoja na baadhi ya wizara zimekuwa zikitoa huduma moja kwa moja kwa wananchi na kuelezea shughuli zinazotekelezwa kwa mujibu wa majukumu yao.

“Maonesho haya yanatoa fursa kwa serikali kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi kuhusu huduma wanazopokea, pamoja na kero zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wakati,” alisema Nkomi

Maonesho hayo pia yameshirikisha baadhi ya sekretarieti za mikoa pamoja na halmashauri, hatua inayowezesha taasisi hizo kuwa karibu zaidi na wananchi wanaozihudumia.

Kwa mujibu wa waandaaji wa maonesho hayo, lengo kuu ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kutumia teknolojia na kushirikisha wananchi katika kujenga serikali bora.

Hata hivyo Kauli mbiu katika wiki hiyo ni "Himiza Matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji"

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI