MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Faraj Abri Asas, amewataka wanachama wa CCM kote nchini kutonyamaza mbele ya kile alichokiita ni upotoshaji unaofanywa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mjini Iringa katika mahafali ya Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Iringa yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Royal Palm, MCC Asas alisema kuwa kuna haja kubwa kwa wana CCM wote kujibu kwa hoja kila upotoshaji unaofanywa dhidi ya mafanikio ya serikali.
“Asilimia kubwa ya hoja zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani ni za kupotosha wananchi. Hawataki kuonesha ukweli kwamba serikali ya CCM chini ya Dkt. Samia imefanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” alisema Asas.
Alisema kuwa hata baadhi ya wapinzani wanaoeneza hoja hizo za kupotosha ni miongoni mwa wanufaika wa kazi nzuri za serikali, ikiwemo huduma bora za afya, mikopo ya elimu ya juu na miundombinu inayowarahisishia shughuli zao za kisiasa.
“Ni unafiki mkubwa kusema hakuna kilichofanyika ilhali wanatumia barabara nzuri, wanatibiwa kwenye hospitali zilizoboreshwa na baadhi yao watoto wao wanasoma kwa mikopo inayotolewa na serikali. Hatupaswi kukaa kimya. Tujibu kwa hoja, kwa ushahidi na kwa kuonesha kazi,” alisisitiza.
MCC Asas alieleza kuwa ana uzoefu mkubwa wa utendaji wa serikali tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi sasa, na anaweza kuthibitisha kwa ushahidi kuwa serikali zote zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, lakini kasi ya Awamu ya Sita ni ya kipekee.
“Toka 1961 hadi leo, kila awamu ya serikali imefanya makubwa. Lakini serikali ya Awamu ya Sita imeonesha ujasiri, dira na uthubutu wa hali ya juu katika kuharakisha maendeleo. Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anatakiwa pongezi za dhati kwa kazi anayoifanya,” alisema.
Kuhusu hoja kwamba serikali inakopa sana, MCC Asas alisema hiyo si hoja ya msingi kwani hakuna nchi duniani inayoendelea bila mikopo. Alisisitiza kuwa mikopo hiyo inachukuliwa kwa misingi ya maendeleo na si kwa matumizi ya anasa.
“Serikali inakopa kwa sababu ina sifa ya kukopesheka. Na fedha zinazokopwa zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo kwa faida ya kila Mtanzania, wakiwemo hao wanaopinga. Hizi si zama za siasa za porojo, tunahitaji hoja na uthibitisho wa matendo,” alisema Asas.
Katika wito wake kwa wanachama wa CCM, MCC Asas alisema kuwa ni wajibu wa kila mwana chama kueleza kwa jamii mafanikio ya serikali, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
“Watanzania wengi wanataka kuona maendeleo. Na wanayaona. Ndio maana Oktoba hii, wote watamchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wa CCM katika ngazi zote tuendelee kuwaambia wananchi kazi zilizofanyika na mipango iliyopo mbele,” alieleza kwa kujiamini.
Katika hatua nyingine, MCC Asas aliwaahidi wanachama wa Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Iringa kuwa atahakikisha changamoto zao za msingi zinashughulikiwa, ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi kama mashine ya kupiga nakala (photocopy) ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Alitumia pia nafasi hiyo kuunga mkono Seneti hiyo kwa kuchangia kiasi cha Shilingi Milioni 2 kwa ajili ya ununuzi wa keki ya mahafali na kuongeza nguvu kwenye mfuko wa Seneti mkoani humo.
“Nawaahidi ushirikiano wa karibu huu ni wakati wa kuwa na vijana makini wenye dira ya kujenga taifa.
Seneti hizi ni taasisi muhimu zinazowatengeneza viongozi wa baadaye, na CCM inathamini sana mchango wenu,” alihitimisha.
Mahafali hayo yaliwahusisha wahitimu kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vilivyopo mkoani Iringa, ambapo walitumia fursa hiyo kujadili masuala ya maendeleo ya kitaifa, nafasi ya vijana katika siasa na mustakabali wa elimu nchini.
0 Comments