Header Ads Widget

VIJANA MBEYA DC WAASWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 2025.


Wananchi wa Jimbo la Mbeya vijijini hususani vijana wamehimizwa kujiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa maelezo kuwa ni haki yao kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa katiba kwa maendeleo yao.

Rai hiyo imetolewa na Gabriel Kilembe afisa kutoka ofisi ya Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza wakati akizungumza na wananchi hususani vijana katika kata ya Inyala waliokusanyika kwa ajili ya bonanza la michezo na kukutanisha vijiji ikiwemo vya Inyala na Darajani.

Kilembe amewapongeza vijana kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wao kuanzia ngazi ya vitongoji ambao wamekuwa chachu ya kusogeza huduma za maendeleo kwenye maeneo yao katika sekta mbalimbali.


Amesema Serikali imefanya mambo mengi ya kimaendeleo ikiwemo usambazaji huduma ya umeme kote vijijini, ujenzi wa shule, uboreshaji huduma za afya, miundombinu ya barabara na maeneo mengineyo hivyo kuwataka vijana kuwa kielelezo kwa kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu ili kuchagua viongozi bora anaodai watasimamishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema pia Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza amekuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo ndio maana ameendelea na ugawaji jezi kwenye timu zaidi ya arobaini katika kata mbalimbali za jimbo hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi wake katika nyanja mbalimbali.

Fredy Mwampashi ni kiongozi wa vijana wa itifaki wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya vijijini, amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza kwani ni kiongozi mahili, msikivu, mchapa kazi na muadilifu ndio maana amepewa nafasi ya kuongoza kamati ya kudumu ya bajeti Bungeni kama mwenyekiti wa kamati hiyo nyeti.

Baadhi ya wananchi waliozungumza nasi wamesema watahakikisha wanashiriki uchaguzi mkuu mwaka huu kwakuwa ni takwa la kikatiba na kueleza kupuuza madai ya baadhi ya wananchi wanaopinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI