Header Ads Widget

TUNDU LISSU KUJITETEA MWENYEWE KESI YA UHAINI, MAHAKAMA YAKUBALI OMBI LAKE

 


Na Matukio Daima App.

Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Lissu, leo Jumatatu Juni 16, 2025, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kuanzia sasa atajitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini inayomkabili, kutokana na madai ya mawakili wake kutotendewa haki na kukosa fursa ya kuzungumza naye faraghani gerezani. Mahakama imekubali ombi lake.

Akizungumza mahakamani mbele ya Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga, Lissu alieleza waziwazi uamuzi wake, akisema, "Kwa haya ambayo nimeyasema mawakili wangu nawashukuru, walipambana sana, walipigana kitaalamu, mlifanya majukumu yenu na mliyafanya kwa usahihi. Hivyo ninaichukua kesi hii mikononi mwangu tena. Kwahiyo Mheshimiwa ‘from now on’ (kuanzia sasa) mimi ndiye nitakaojibizana na hao mawakili wa serikali."

Lissu alibainisha kuwa mojawapo ya sababu kuu za uamuzi wake huo ni kukosa nafasi ya faragha na mawakili wake akiwa mahabusu. Amekuwa mahabusu kwa siku 68 bila mawakili wake kuruhusiwa kumuona kwa faragha na kuwasiliana naye kwa uhuru, jambo ambalo alilieleza Mahakama kama kukosekana kwa haki.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga alitoa uamuzi mdogo kuruhusu ombi la Lissu. "Kuanzia sasa hoja zitakuwa zinajibiwa kati ya upande wa Mawakili wa Jamhuri na mshitakiwa mwenyewe mpaka pale atakaposema vinginevyo, kwamba naomba mawakili wangu warudi," alisema Hakimu Kiswaga.

Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni. Uamuzi huu wa Mahakama unamaanisha kuwa kuanzia sasa, Lissu atakuwa akishiriki moja kwa moja katika mabishano ya kisheria na mawakili wa serikali bila uwakilishi wa mawakili wake wa awali, isipokuwa atakapoamua vinginevyo.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI