Header Ads Widget

TACOGA 1984 YATOA MAFUNZO KWA WASHAURI WA WANAFUNZI KUIMARISHA HUDUMA ZA USHAURI VYUONI

 

Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984) kimetoa mafunzo kwa washauri wa wanafunzi kutoka vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya kati, vyuo vya ufundi pamoja na viongozi wa serikali za wanafunzi, kwa lengo la kuwaongezea uelewa na uwezo wa kuwapa ushauri wanafunzi na kuwasimamia kwa tija.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Eden jijini Mbeya, yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo afya ya akili, afya ya uzazi pamoja na mbinu bora za ushauri kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Akifunga mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya (CUoM), Profesa Romuald Haule, amewasisitiza washiriki kutumia mbinu rafiki katika kutoa ushauri badala ya kutumia njia ngumu zinazoweza kuwatenga au kuwavunja moyo wanafunzi.


"Niwahimize kutumia njia zenye kujenga mahusiano mazuri na wanafunzi. Ushauri siyo adhabu, bali ni msaada unaolenga kubadilisha maisha ya mtu kwa upendo na uelewa," amesema Prof. Haule.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TACOGA 1984, Bi. Sophia Nchimbi, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za chama hicho kuhakikisha kuwa washauri wa wanafunzi wanakuwa na ujuzi wa kisasa unaoendana na changamoto za sasa zinazowakumba wanafunzi.


"Masuala ya afya ya akili na uzazi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanafunzi wengi leo hii. Hivyo tumelenga kuwajengea uwezo washauri ili waweze kuwasaidia wanafunzi katika maeneo hayo kwa weledi na ufanisi," amesema Nchimbi.

Mafunzo hayo yanatajwa kuwa sehemu ya mikakati ya TACOGA 1984 katika kuboresha huduma za ushauri na uongozi kwa wanafunzi katika taasisi za elimu nchini.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI