Header Ads Widget

SERIKALI YAONYA VIJANA MATUMIZI MABAYA YA MITANDAO YA KIJAMII.

 


 


Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App


MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewaonya vikali vijana wa vyuo vikuu dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa baadhi yao wamekuwa wakitumiwa kuandika na kusambaza taarifa zinazolenga kuichafua serikali na kuigombanisha na wananchi. 


Ametoa wito kwa vijana kutumia majukwaa haya ya kidijitali kwa kujielimisha, kujifunza na kujitangaza kibiashara badala ya kujiingiza kwenye maudhui hatarishi yanayoweza kuwaingiza matatizoni kisheria.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msigwa alikumbusha kuwa sheria ipo na vyombo vya dola vinaendelea kuwachukulia hatua wale wanaokiuka masharti ya matumizi ya mitandao.


Amesema kutojua sheria siyo kisingizio cha kuivunja, hivyo vijana wanapaswa kuwa waangalifu wanapochapisha maudhui mtandaoni.


Katika hatua nyingine, Msigwa alitangaza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku saba katika mikoa ya Simiyu na Mwanza kuanzia Juni 15. Ziara hiyo inalenga kuzungumza na wananchi pamoja na kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.


Miongoni mwa miradi hiyo ni Daraja la Kigongo–Busisi ambalo limekamilika kwa asilimia 100 na litazinduliwa rasmi Juni 19. Mradi huo mkubwa wa miundombinu umeelezwa kuwa ni sehemu ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia.


Baada ya ziara ya mikoani, Rais Samia pia atafanya ziara maalum ya kikazi katika nchi ya Msumbiji na Visiwa vya Comoro kufuatia mialiko maalum aliyopokea kutoka kwa viongozi wa mataifa hayo.


Kuhusu hali ya uchumi, Msigwa alisema Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji zinatarajia kuwasilisha bajeti kuu ya serikali ambayo kwa mara ya kwanza itatolewa kwa kutumia fedha za ndani pekee. Ameeleza kuwa bajeti hiyo itakuwa ya kihistoria kwa kuwa itatoa mwelekeo wa bajeti ya uchaguzi ujao.


Aidha, serikali imepokea gawio la shilingi trilioni 1.28 kutoka kwa mashirika ya umma, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa serikali wa zaidi ya trilioni 86 katika sekta hiyo. Msigwa amesema ongezeko hilo ni ushahidi wa mafanikio ya utekelezaji wa falsafa ya 4R iliyoanzishwa na Rais Samia.


Kwa upande wa ujenzi wa mji wa serikali awamu ya pili katika eneo la Mtumba, Msigwa amesema kazi hiyo imefikia asilimia 90 huku majengo sita kati ya 34 yakiwa tayari yamekamilika na kuanza kutumiwa na wizara husika. Ujenzi wa miundombinu kama barabara na umeme unaendelea kwa kasi.


Akiwaelezea mafanikio ya maendeleo, Msigwa ameeleza kuwa miundombinu ya umeme wa ardhini imefikia asilimia 59, huku kazi ya upandaji miti ikiwa imehusisha miti 233,000. Kamera za usalama pia zimefungwa kwa asilimia 55, hatua ambayo inalenga kuongeza usalama na ustawi wa mji wa serikali.


Msigwa amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi, kuhakikisha usalama wa raia na kutumia rasilimali za ndani katika maendeleo ya taifa, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu kwa kufuatilia bajeti na kutoa ushirikiano kwenye miradi mbal. imbali ya maendeleo.


Mwisho. 









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI