Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amewashukuru wanachama wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) kwa kumpa ushirikiano kwa kipindi chote baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Licha ya kuwashukuru wanachama hao ameelezea namna alivyotekeleza ilani ya uchaguzi kwa kipindi kinachokwenda kumalizika.
Katika kituo chake cha kwanza akiwa Kata ya Mshikamano amesema ushirikiano alioupata kutoka kwa wanachama na wananchi ndio uliopelekea kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Amesema alishasoma utekelezaji huo na mengi yanaonekana na ruhusa aliyoipatabungeni kutoka kwa Spika ni kuja kuwashukuru na kuwaaga na muda ukifika wataonana tena.
Mbunge huyo amesema kwenye elimu, afya, maji, miundombinu na masuala ya kijamii yamefanyika na kuondoa kero na changamoto kwa wananchi.
Mathayo amesema kwa kuwa wananchi wameonyesha imani kwake na kumuomba kugombea tena atafanya hivyo muda ukifika kwa kuwa bado anayo nguvu na ari ya kuwatumikia
" Hii ni siku ya pili ya ziara yangu ya xiku 4 kuja kuwashukuru kwa kunipa ushirikiano kwa kipindi cha miaka 5 ya uongozi wangu ndani ya jimbo la Musoma mjini.
" Wapo wanaopita na kueleza kwamba hakuna jambo lililofanyika wapuuzwe kwa kuwa mambo yanaonekana kwa kila mmoja",amesema.
Akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani wa Kata na viti maalum kwenye Kata hizo za Mshikamano,Buhare,Iringo na Kigera kwa nyakati tofauti wamempongeza mbunge huyo kwa namna alivyochapa kazi.
Kwa upande wao madiwani wa viti maalum Amina Masisa, Alieth Kumila,Meryciana Masasi na Naibu Meya Naima Minga wamesema wameshirikiana vyema na mbunge huyo na kuomba wanapokwenda kumchagua mbunge Mathayo wawakumbuke na nao.
Diwani wa Kata ya Kigera Alex Nyabiti amesema maendeleo makubwa yamefanywa zikiwemo huduma za afya,maji,miundombinu na kwenye elimu ni Kata ya kwanza kujengwa shule ya gorofa.
Amesema muda ukifika wasiache kumchagua mbunge Mathayo kwa kazi nzuri aliyoifanya lakini yeye pia wasimsahahu kwa kuwa ameshirikiana vyema na wananchi wa Kata ya Kigera katika shughuli za maendeleo.
Mwisho.
0 Comments