Na,Jusline Marco;Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, amesema ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mkoa wa Arusha ni kuona mkoa huo unakuwa kitovu cha utalii na uchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo, hasa kupitia sekta ya utalii.
Makonda ameyasema hayo katika kikao chake na viongozi wa mashirika ya reli na bandari waliotembelea Mkoa huo,ambapo ameeleza kuwa Rais Samia amedhamiria kwa vitendo kuleta maendeleo katika Mkoa wa Arusha, jambo linalodhihirika kupitia miradi mikubwa inayoendelea kwa sasa, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa na ukumbi mkubwa wa mikutano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Reli Tanzania Ally Karavina ameeleza kuwa wameona umuhimu wa kukagua reli ya kutoka Arusha hadi Dar es Salaam, na kufikiria namna ya kuunganisha njia hiyo hadi Tanga na tayari wamepata mradi wa ukarabati wa reli hiyo ili kuongeza kasi ya usafiri wa treni kufikia wastani wa kilomita 70 kwa saa.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plusduce Mbosaa ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Bandari Kavu jijini Arusha na kuongeza kuwa wako tayari kutoa vibali kwa mtu au taasisi yoyote yenye nia ya kuwekeza kwenye mradi huo hatua itakayorahisisha shughuli za usafirishaji na kuongeza ufanisi katika biashara.
0 Comments