NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Ikiwa imebaki siku chache kuwasilisha Kwa Rais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan katika ziara ya kikazi Jijini Mwanza inayotarajiwa kufanyika kuanzia juni 19 hadi 21 mwaka maandalizi ya kiusalama.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani hapa Wilbroad Mtafungwa amesema kuwa jeshi la polisi limejipanha kudhibiti vitendo vya kihalifu na kuratibu usalama kwa wageni na viongozi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi watakaoshiriki katika shughuli za kitaifa wakati wa ziara hiyo.
Mtafungwa ameeleza kuwa askari wa usalama wameongezwa katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa, maeneo ya wazi yatakayotumika kwa mikutano, pamoja na barabara kuu zitakazopitisha misafara rasmi ya viongozi.
“Tunachukua hatua za tahadhari ili kuhakikisha mazingira yote ni salama. Usalama si jukumu la Polisi pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kwa kutoa taarifa na kufuata taratibu zilizowekwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika kuhakikisha usafiri unafanyika kwa utaratibu na bila usumbufu, Jeshi la Polisi limeanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu kwa madereva kuhusu njia mbadala, muda wa kufungwa kwa baadhi ya barabara na namna bora ya kuepuka msongamano. Kampeni hiyo inaanza rasmi tarehe 17 Juni.
Jeshi hilo pia limewaomba wananchi kujiepusha na vitendo vya kuvuruga amani ikiwemo kusogelea misafara ya viongozi bila ruhusa, kupiga honi au kutumia magari yenye sauti kubwa karibu na maeneo ya mikutano.
Wakati huohuo, vikosi vya doria vya pikipiki, magari na askari wa miguu vimeimarishwa ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yenye shughuli nyingi kama masoko, vituo vya mabasi na sehemu za burudani, hasa nyakati za usiku.
Ziara ya Rais Samia inatarajiwa kuibua shughuli nyingi za maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, na hivyo usalama wa raia na wageni ni jambo linalopewa kipaumbele cha juu na vyombo vya dola.
0 Comments