Mwanaume mmoja ameuawa na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia kando ya barabara ya Moi mjini Nairobi wakati wa maandamano ya kutaka haki ya Albert Ojwang na kujiuzulu kwa Naibu Inspekta Mkuu Eliud Lagat.
Katika video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, maafisa wawili wa polisi walijifanya kama wanampita mwanamume huyo alipokuwa amesimama, ambaye alikuwa anauza barakoa alizozibeba mkononi kabla ya kumgeukia.
Kisha wakaanza kumpiga kabla ya mmoja wao kuinua bunduki na kumfyatulia risasi kwa umbali wa karibu mno.
Mwanamume huyo papo hapo, alianguka chini, akawa hawezi kusonga huku akiwa bado ameshika mfuko wake wa barakoa nyeusi alizokuwa anauza, kisha maafisa hao wakaondoka, wakielekea upande uleule waliotoka.
Baada ya muda mfupi, kikundi cha waandamanaji kilikimbilia upande ambao mwanamume huyo alikuwa ameanguka, na kumpata akiwa hana uhai.
"Alikuwa akiuza barakoa wakati watu walipoanza kukimbia, akabaki peke yake wakati sisi wengine tukikimbia. Tumeona mmoja wa maafisa akimpiga risasi na baada ya hapo akaanguka chini," mwenzake mwathiriwa aliwaambia waandishi wa habari.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), Faith Odhiambo, amesema hali hiyo "Haikubaliki", baada ya kuona video inayosambaa.
Kiongozi wa chama cha People's Liberation Party Martha Karua pia amelaani vikali mauaji ya mwanamume huyo na polisi.
Akijibu video ambayo inaonekana kuonyesha wakati ambapo mwanamume huyo aliuawa, Karua aliita mauaji hayo kuwa "mauaji mengine ya kiholea".
"Ni vifo vingapi vitatokea ili muache kufanya hivi," Karua aliuliza swali hilo kwa Huduma ya Taifa ya Polisi.
Mauaji ya mwanamume huyo yamezidisha hasira miongoni mwa waandamanaji ambao wanaandamana kwa sababu ya kifo cha Albert Ojwang, mwanablogu aliyekufa mikononi mwa polisi huku wakimtaka naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Eliud Lagat ajiuzulu.
Lagat amejiondoa kwenye cheo chake kupisha uchunguzi unaoendelea.
0 Comments