Header Ads Widget

WATUMISHI WATAKIWA KUZINGATIA WEREDI KUEPUKA HOJA ZA MKAGUZI WA SERIKALI.

 

KATIBU Tawala mkoa wa Katavi, Albert Msovela, akiongea kwenye Baraza Maalumu la wilaya ya Tanganyika kwa ajili ya kujadili hoja za ukaguzi wa Hesabu za Serikali.

Na Mwandishi wetu, Matukio Daima app.


KATIBU Tawala mkoa wa Katavi, Albert Msovela amewataka watumishi katika mkoa huo kuzingatia weredi katika utendaji wa kazi pamoja na kuzingatia sheria ili kuondoa hoja zisizo na mashiko katika ukaguzi wa hesabu za mkaguzi mkuu wa serikali na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.


Akizungumza katika baraza maalumu la madiwani la kupitia na kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika leo Juni 17, 2025 amesema hoja zitakazokuwa zikiibuliwa zitajibiwa na wakuu wa idara ili kuondoa uzembe wa kutokuzingatia sheria.


"Inasikitisha kwamba tunapata hoja sababu mtu alifanya manunuzi hakupata risiti ya EFD maana yake hakufata sheria, sheria zipo na mwenye kuisimamia hiyo sheria ni sisi watumishi tukifanya hivyo tutawasaidia sana wananchi hizi kero na changamoto zinazozungumzwa hazitakuwepo," Amesema Msovera.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni, 2024. Kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 katika baraza hilo Kasela Lyoba kutoka ofisi ya mdithibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amesema imepata hati safi ya ukaguzi.


Amesema mwaka wa fedha 2023/24, mkaguzi alitoa hoja 38 za Ukaguzi ambapo hoja 18 zilihusisha utendaji wa Halmashauri na hoja 20 zilihusisha usimamizi na utekelezaji wa miradi pamoja na mifuko mbalimbali. Aidha Halmashauri ilikuwa na hoja 16 za miaka ya nyuma hivyo kufanya jumla ya hoja kuwa 54


"Baada ya kupokea taarifa ya hoja, Menejimenti imefanya jitihada kutekeleza mapendekezo ya mkaguzi ambapo hadi kufikia hii leo. Hoja 32 kati ya hoja 54 zimetekelezwa kikamilifu na zimependekezwa kufungwa huku hoja 22 zilizosalia zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji" Amesema.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu akizungumza na madiwani katika baraza hilo amewataka kuwa mabarozi wazuri wanapomaliza ungwe yao ya uongozi kwa kuhakikisha wanawaeleza wananchi mambo ambayo serikali imekuwa ikifanya kwa maendeleo yao.


Amesema Rais ameleta fedha nyingi katika kukamilisha miradi ya maendeleo katika sekta ya afya, maji, Elimu, barabara na kila nyanja ndivyo vinavyofanya wananchi watembee kifua mbele wakijivunia maendeleo.


Mwisho.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI