Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo ameeleza sababu za kumchagua Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
Sababu za kumchagua amezieleza ni pamoja na kutoa fedha nyingi zilizoweza kutekeleza miradi ya elimu,afya,maji,miundombinu na masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Kauli hiyo ameisema leo juni 20,2025 Kijijini Murangi wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020,2025 kwenye Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Musoma Vijijini.
Amesema kuanzia kipaumbele cha kwanza cha elimu kati ya vipengele 5 serikali ya awamu ya 6 chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi ambazo zimetekeleza miradi ya elimu kuanzia ujenzi wa shule mpya na kuongeza madarasa.
Profesa Muhongo amesema wakati anashika nafasi ya ubunge 2020 Jimbo la Musoma Vijijini kulikuwa na shule za sekondari 14 na sasa zipo shule 30 za serikali zikiwemo 2 za binafsi.
Amesema licha ya uwepo wa shule hizo 18 zinajengwa na ifikapo julai mosi mwaka huu High Schools 2 za masomo ya sayansi za Suguti na Mugango zitafunguliwa.
Amesema elimu ni suala la msingi na hakuna urithi uliokuwa bora kama kumuwezesha mtoto wa jimbo la Musoma Vijijini kupata elimu.
Mbunge Muhongo amesema ujenzi wa shule ndani ya jimbo kwa miaka 5 huanza kujengwa kwa nguvu za wananchi na harambee zinazoendeshwa na mbunge na baadae serikali kuu uchangia ukamilishwaji wake.
Kwenye sekta ya afya amesema serikali katika kipindi hicho imetoa kiasi cha bilioni 5.7 ambazo zimewezesha ujenzi wa zahanati,vituo vya afya na hospitali ya Wilaya ya Musoma Kwikonero Kata ya Suguti.
Utekelezaji kwenye sekta ya maji Muhongo ameelezea vijiji vyote 68 vina miradi ya maji ya bomba kutoka ziwa Victoria pamoja na uchimbaji wa visima ambapo zaidi ya bilioni 22 zimewekezwa na usambaji umefikia asilimia 90.
" Kwa yale ambayo yametekelezwa ndani ya jimbo letu chini ya serikali ya awamu ya 6 chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan sisi Musoma Vijijini tutamchagua kwa asilimia 100.
" Fedha nyingi tumeletwa kwenye miradi ya elimu,afya,maji,miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi",amesema.
Amesema kwenye barabara nyingi zimefunguliwa na barabara kuu ya Musoma-Murangi-Busekera ipo kwenye bajeti kwaajili ya ujenzi wa kilometa 40 na tayari kilometa 5 zimeshajengwa kwa kiwango cha lami na kufungwa taa za barabarani
Kuhusu kuwezesha wananchi kiuchumi amesema shughuli za kilimo,uvuvi kutumia vizimba vilivyowezeshwa na mikopo ya serikali na ufugaji imesaidia kuwezesha wananchi kiuchumi.
Kilimo cha umwagiliaji kupitia bonde la Bugwema mbunge Muhongo amesema litakuwa suruhisho la njaa kwa wananchi na kilimo biashara.
Kwenye sekta ya michezo na utamaduni hakuisahau namna ilivyofanikiwa kutekelezwa kwenye kipindi hicho na kudai itaendelezwa kwenye kipindi kingine endapo atachaguliwa tena kwenye nafasi hiyo na kuwa mwakilishi wa jimbo la Musoma Vijijini.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 2000 Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini Denis Ekwabi kazi zilizofanywa na mbunge Profesa Sospeter Muhongo zinaonekana kwa macho na ameitendea haki ilani.
Amesema wajumbe wameona na wamesikia hivyo wakati ukifika watakwenda kulipa kwa kile kilichofanyika.
Licha ya kusomewa utekelezaji wa ilani wajumbe wa Mkutano Mkuu wamekabidhiwa vitabu na mbunge hiyo vinavyoelezea utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha mwaka 2020/2025.
0 Comments