Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ametangaza kusitishwa kwa kipindi cha maombolezo ya kitaifa cha rais wa zamani Edgar Lungu, baada ya mvutano kuzuka kati ya serikali na familia kuhusu mipango ya mazishi yake.
Tangazo hilo limekuja siku moja tu baada ya familia ya Lungu kughairi kurejeshwa kwa mwili wake kutoka Afrika Kusini, hatua iliyozua sintofahamu nchini.
Awali, serikali ilikuwa imepanga kumpokea marehemu kwa heshima zote za kijeshi siku ya Jumatano, huku mipango ikiwekwa ya mwili wake kulala nyumbani kwake kabla ya mazishi yaliyopangwa kufanyika Jumapili na Jumatatu.
Hata hivyo, familia ilidai kuwa serikali ilikiuka makubaliano ya awali kuhusu mipango ya mazishi, na hivyo kusitisha usafirishaji wa mwili.
Rais Hichilema amesema serikali yake imejitahidi kufanya mazungumzo na familia ya marehemu, lakini sasa imefikia hatua ya kufanya uamuzi mgumu ili nchi irejee katika hali ya kawaida.
Alisisitiza kuwa Lungu, kama rais wa zamani, ni mali ya taifa na anapaswa kuzikwa kwa heshima zote nchini Zambia. Chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF), ambacho Lungu alikiongoza hadi kifo chake, kimeunga mkono msimamo wa familia, kikishutumu serikali kwa kugeuza tukio la huzuni kuwa jukwaa la siasa.
Viongozi wa kidini na makundi ya kiraia wametoa wito wa maelewano ya haraka ili kulinda heshima ya taifa. Edgar Lungu aliongoza Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021 kabla ya kushindwa katika uchaguzi wa urais.
Alifariki dunia mapema mwezi huu akiwa nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Licha ya kustaafu siasa kwa muda, alijitosa tena na kuendelea kuwa sauti muhimu katika siasa za Zambia.
0 Comments