Header Ads Widget

MAJINA 126 YA WAFUNGWA YAPENDEKEZWA NA BODI YA TAIFA YA PAROLE,KUWASILISHWA KWA WAZIRI MWENYE DHAMANA

 

Na Lilian Kasenene,Morogoro

Matukio Daima Media

BODI ya Taifa ya Parole imependekeza wafungwa 126 kunufaika na utaratibu wa Parole kwa mwaka huu kwa mujibu wa sheria ya bodi hiyo sura ya 400.

Kamishna Jenerali wa Magereza CGP Jeremiah Katungu ambaye ni katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole alisema hayo mjini Morogoro baada ya bodi hiyo kukutana.

CGP alisema Sheria hiyo inatoa fursa kwa wafungwa waotumikia kifungo magerezani kutoka na kwenda kwenye jamii kumalizia sehemu ya vifungo vyao wakiwa kwenye jamii.

Wafungwa hao 126 waliopendekezwa, wamo wanaume 123 na wanawake watatu na ni kati ya majina 159 yaliyopendekezwa kutoka bodi za parole za mikoa ambapo wafungwa 33 hawajapendekezwa..

Alisema majina hayo yatawasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi ambaye kwamujibu wa sheria ndiye mwenye maamuzi ya mwisho.

“Bodi ya taifa ya Parole baada ya kupendekeza haya majina na kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi,Waziri hutoa maamuzi ya mwisho ya kuridhia ama kutokuridhia wafungwa hawa waweze kunufaika na utaratibu huu,'alisema CGP Katungu.

Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza alisema yapo masharti ambayo yameainishwa katika sheria husika juu ya namna wafungwa wanaweza wakafikiriwa kunufaika na utaratibu huo wakiwemo wafungwa wanaotumikia kifungo cha kuanzia miaka minne na kuendelea.

Aliaja masharti mengine kuwa ni  lazima wafungwa wawe wametumikia moja ya tatu ya vifungo vyao magerezani na kwamba utaratibu huo hauwahusu wafungwa waliofungwa maisha ama waliotenda makosa ambayo hayaja ainishwa kwenye sheria hii ikiwemo wanaotumikia vifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha,makosa ya kujiaminiana na wale wanaotumikia vifungo kwa makosa ya madawa ya kulevya.

Kamishna Jenerali huyo mwenye dhamana na Jeshi la Magereza akasema Wafungwa hao kimsingi hawaruhusiwi kufikiriiwa na utaratibu huo kwa sababu imekatazwa katika sheria husika na kwamba utaratibu huo umekuwa na manufaa makubwa katika jukumu zima la urekebishaji wa wahalifu magerezani ikiwemo kuihusisha jamii katika jukumu la urekebishaji wa wafungwa.

“Kama mnavyofahamu, mhalifu alikuwa kwenye jamii na baada ya kutenda kosa akaingia gerezani, na jukumu la magereza ni kumbadilisha mwenendo na tabia lakini kumrekebisha kwa kumpa ujuzi maarifa na elimu na mwisho wa siku akimaliza kifungo lazima arudi tena kwenye jamii."alisema

"sasa jamii ina mchango mkubwa katika jukumu la urekebishaji kwa wahalifu na utaratibu huu pia unatoa fursa ya jamii kushiriki katika kumrekebisha mfungwa kwa maana ya mfungwa akiwa nje anakwenda kwenye jamii anamalizia sehemu ya kifungo ambacho kimebaki,”alisisitiza CGP.

Alitaja faida nyingine ya utaratibu huo kuwa husaidia kupunguza gharama za kuwahudumia wafungwa wakiwa magerezani ambapo mfungwa akiwa gerezani Serikali hutoa huduma mbalimbali ikiwemo chakula, mavazi huduma za matibabu na huduma nyingine.

Faida nyingine ni mwenendo na tabia ya wafungwa kuwa mzuri wakiwa magerezani kwani  ili mfungwa anufaike na utaratibu wa parole  ni lazima mwenendo wake gerezani uzingatie tabia njema na mwenendo mzuri ndio apatenafasi nzuri ya kufikiriwa kwa hiyo utaratibu huo husaidia kuimarisha mienendo ya wafungwa ili wawe na matarajio kwamba watafikiliwa kwenye utaratibu wa parole na kwenda nje kutumikia sehemu ya kifungo chao kwenye jamii.

Kuhusu wafungwa wanaotolewa kwa msamaha wa Parole kama wapo waliohusika na makosa na kurejeshwa magerezani, CGP Katungu alisema kwa mujibu wa utaratibu mfungwa akitoka nje kwa utaratibu wa parole huwa anaendelea kufuatiliwa mienendo na tabia zake akiwa kwenye jamii na endapo atakiuka taratibu zilizopo husitishwa  kwenye utaratibu wa Parole kwa mujibu wa sheria na kurudishwa gerezani.

“Lakini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuna mfungwa anayetumikia kifungio jwa taratibu za parole ambaye alikiuka  taratibu na kurudishwa gerezani,wafungwa wote ambao wamekuwa wakitoka kwa utaratibu huu wanakidhi vigezo kwa kuwa na mienendo mizuri kwenye jamii na hatimaye wanamaliza kifungo ndani ya utaratibu husika na kuhusu idadi ya waliojadiliwa kuwa ni ndogo, huwa kwa kawaida mchakato wa mapendekezo huanzia kwenye magereza husika kwa kuangalia waliokidhi vigezo ambao kwanza hujadiliwa na bodi za parole za mikoa na baadaye taifa,”alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu,aliwasihi wafungwa kubadili tabia na mienendo yao magerezani ili kunufaika na utaratibu huo kwani sheria ya Parole imeweka vigezo vya wafungwa awanaoweza kunufaika kwa kuruhusiwa kumalizia vifungo vyao kubwa ikiwa ni mabadiliko ya mwenendo wa tabia zao magerezani.

“Nitoe wito kwa wafungwa ambao wako magerezani watambue kuwa magereza ni sehemu ya kurekebisha tabia, waliteleza wakatiwa hatiani, wakaadhibiwa kutumikia vifungo magerezani lakini bado kuna fursa, Magereza sasa ni chombo chetu cha kurekebisha tabia na mienendo ya wafungwa, watumie vizuri fursa hii  kujifunza na kurekebisha mienendo yao na wakirekebika basi wanaweza kunufaika”alisema DPP Mwakitalu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI