Header Ads Widget

MAJI ZIWA VICTORIA KUCHUKULIWA SAMPULI ILI KUFANYIWA UTAFITI KUJUA UBORA WAKE

 

Na Chausiku Said, Mwanza

Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kwa kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatarajia kufanya utafiti wa kisayansi wa pamoja kwa ajili ya kuchunguza ubora wa maji ya Ziwa Victoria.

Utafiti huo, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), utahusisha uchukuaji wa sampuli za maji kutoka eneo la ziwa kwa upande wa Tanzania, na Sampuli hizo kufanyiwa uchambuzi ili kubaini ubora wa maji katika ziwa Victoria.

Akizungumza katika kikao cha wataalamu kilichofanyika juni 4 2025 Jijini Mwanza, Naibu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la ziwa Victoria (LVBC), Coletha Ruhamya, alisema kuwa utafiti huu ni hatua muhimu kuelekea kutengeneza sera bora za kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria, ambalo linategemewa na mamilioni ya watu kwa matumizi ya kila siku na shughuli za kiuchumi.

“Maji yanaweza kuonekana safi kwa macho, lakini bila uchunguzi wa kisayansi hatuwezi kujua hali halisi. Huu ni utafiti muhimu unaopaswa kufanyika mara kwa mara, kila baada ya miezi mitatu au sita, ili kutoa taswira sahihi ya ubora wa maji,” alisema Ruhamya.

 “Tunapokuwa na takwimu za pamoja, tunakuwa na uelewa wa pamoja, na hapo ndipo tunapoweza kufanya uamuzi wa pamoja wa kulinda ziwa letu. Hii ni hatua ya kisayansi yenye umuhimu wa muda mrefu,” aliongeza Coletha Ruhamya.

Kwa upande wake, Omary Idd, mshauri wa kiufundi kutoka GIZ, alisema kuwa shirika hilo liliamua kufadhili mradi huo baada ya kubaini kuwa hakuna maendeleo endelevu yanayoweza kufikiwa bila data sahihi za kisayansi kuhusu hali ya mazingira.

“Uchafuzi wa ziwa si jambo la kubashiri. Tunahitaji takwimu sahihi ili kubaini chanzo halisi cha tatizo na kupanga hatua stahiki. Utafiti huu utasaidia kuunda miradi ya kudhibiti uchafuzi kabla haujaleta madhara zaidi,” alisema Idd.

Idd ameeleza kubwa uchunguzi huo pia ni sehemu ya programu pana ya kujenga uwezo wa wataalamu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mafunzo ya siku tatu yameanza rasmi Juni 4 kwa wataalamu wa maji, mazingira na maabara, ambao watatumia teknolojia mpya kuchambua sampuli za maji kwa viwango vya kimataifa.


Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, amesema kuwa mara ya kwanza, nchi tatu zinashirikiana kwa kiwango cha juu kufanya tathmini ya pamoja ya ubora wa maji, jambo linaloimarisha ufanisi wa utunzaji wa rasilimali hiyo ya pamoja.

“Programu ya uchukuaji wa sampuli za pamoja itasaidia kuelewa ni maeneo gani yanaathirika zaidi na kwa sababu zipi. Tukifahamu hilo, tutaweza kuelekeza nguvu katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi,” alisema Shinhu 

Shinhu amesema kubwa utafiti huu unatarajiwa kutoa taarifa zitakazosaidia serikali za nchi wanachama kutunga sera mpya au kurekebisha zilizopo, sambamba na kubuni miradi ya kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria kwa ufanisi zaidi.

Ziwa Victoria ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani na tegemeo kuu la maji, uvuvi na usafirishaji kwa zaidi ya watu milioni 40 wanaoishi katika bonde lake.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI