Header Ads Widget

MAAFISA 11 WA POLISI SONGWE WAFUNDWA KUZINGATIA MAADILI.

 

Na Matukio Daima Media 

Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban, amewataka Maofisa 10 na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi 01 kwenda kuvitendea haki vyeo vyao walivyovipata kwa jamii kwa kuyaishi na kutekeleza mambo yenye tija ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu hayo wakiwa na hofu ya Mungu ili kutoa haki na kuyafanya kwa vitendo yale yote waliyofundishwa wakiwa mafunzoni.



Rai hiyo imetolewa Juni 16, 2025 katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe wakati akiongea na Maofisa na Mkaguzi ambao walihitimu mafunzo yao ya uongozi Juni 09, 2025 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), mafunzo yaliyofungwa na Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.


"Mnapotekeleza majukumu yenu katika kazi za kila siku fanyeni huku mkiwa na hofu ya Mungu bila kusahau kufanya kazi kwa nidhamu kwa kuwatendea haki wateja wa ndani na nje ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo na kuwa waadilifu bila kuwa na muhali na mtu yoyote ili jamii iendelee kuwa salama" amesema ACP Akama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Johnny Maro amewataka Maofisa hao kwenda kusimamia nidhamu kwa askari waliochini yao pamoja na ufuatiliaji wa majalada ya kesi na kuyakamilisha kwa wakati kwa kufuata utaratibu ili jamii iendelee kuliamini Jeshi la Polisi na kuweza kupata taarifa fiche za uhalifu na wahalifu kwa lengo la Mkoa wa Songwe kuendelea kuwa salama.


Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Joseph Bukombe, amewataka maofisa hao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uhalifu na ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya Jeshi la Polisi nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI