Header Ads Widget

LIBERATA MULAMULA, MWANADIPLOMASIA ALIYEKUWA KWENYE HARAKATI ZA KUTAFUTA AMANI DRC


 Mfahamu Balozi Leberata Mulamula mwanadiplomasia Mbobevu aliyehatarisha maisha yake kuhakikisha makundi ya wapiganaji wenye silaha mashariki ya Congo, wanakaa meza moja kuzungumzia amani.

Ametumikia maisha yake yote ya ajira, Wizara ya Mambo ya nje na kupanda vyeo kutoka Afisa wa Kawaida Mpaka Waziri

''Unavyoiona hali ilivyo katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sasa,ndio hali ambayo niliikuta mimi wakati nilipoteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa sekretarieti ya maziwa makuu''

Ni katika mazungumzo yangu na Balozi Liberata Rutegaruka Mulamula, Mwanadiplomasia kutoka Tanzania ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya nchi za Nje, Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico pamoja na Katibu Mtendaji wa sekretariet ya Kanda ya Maziwa Makuu -ICGLR.

Balozi Mulamula anasema anasikitishwa na hali ya mashariki ya Congo ambapo hivi karibuni kulitokea mapigano kati ya waasi na jeshi la serikali ambapo watu wengi waliuawa na wengine kuyakimbia makazi yao.

''Lengo la kuanzishwa kwa mchakato wa maziwa makuu lilikuwa ni tumalize migogoro yetu kwa njia za mazungumzo, lakini unaona mazungumzo yanaendelea lakini vita vinaendelea na watu wanazidi kuuawa, watu wanakimbia makazi yao.. Najiuliza tunashindwa wapi?''

Wakati akihudumu nafasi hiyo makazi yake yalikuwa Bujumbura Burundi, na wakati huo hali katika Eneo la maziwa makuu haikuwa sawa, Burundi ikiwa imetoka tu kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1993 mpaka 2005. Rwanda nako hali kadhalika ilikuwa ikiponya majeraha ya mauaji ya kimbali. Mashariki mwa Congo nako mapigano yalikuwa yamepamba moto.

''Huwezi kuwa umepewa kazi halafu ukakaa tu Bujumbura, sehemu nyingine huwezi kwenda. Nakumbuka mama mkwÄ™ wangu alinipigia simu akasema tumesikia kuna vita Congo…, urudi nyumbani kama uko huko…, nikamwambia Mama hii ndio kazi iliyonileta huku''

Kazi yake ilimfanya balozi Liberata Mulamula kuishi katika uwanja wa mapambano.

''Bila ya shaka nilikuwa na hatarisha maisha yangu, lakini unasema niko kazini kuhakikisha vikundi vya wapiganaji vinakubali kuzungumza''



Juni 21 mwaka 2008 mataifa manane kati ya 11, wanachama wa Taasisi ya Mkutano wa Kimataifa ya Kanda ya Maziwa Makuu yaliridhia mwafaka juu ya Usalama, Utulivu na Maendeleo katika Maziwa Makuu.

Mataifa hayo ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kenya, Jamhuri ya Kongo, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Lengo pia la kuanzishwa kwa mchakato huo ni kwa ajili ya makundi yenye silaha yaliyokuwa yakipigana kuweza kuzungumza ili amani ipatikane.

''Mimi ndio nilikuwa na wajibu wa kusimamia kuhakikisha mazungumzo yanaendelea, wakati huohuo mapigano yakiwa yanaendelea..Kwa hiyo ndio hivyo nilikuwa nikihatarisha maisha yangu lakini ndio jukumu ambalo nimepewa''.

Balozi Mulamula anasema ilikuwa changamoto kubwa kwake lakini hata hivyo, baada ya kuhudumu kwa miaka sita na kufanikisha yale aliyojaaliwa kanda ikatulia.

''Nikasema moyoni kuwa changamoto inaweza kuwa fursa japo kwa kweli hali ilikuwa tete, lakini mpaka naondoka hali ilikuwa tulivu kabisa..''.

Marais kama vile Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na Olesegun Obasanjo wa Nigeria waliweza pia kushiriki katika mazungumzo ya amani na makundi ya wapiganaji..

Pengine kuwa Mwanadiplomasia aliyebobea kuliweza pia kumrahisishia kazi yake.

Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Shahada ya Sayansi ya Siasa- (Political science) akijikita zaidi katika taaluma ya Mahusiano ya kimataifa na utawala. Moja kwa moja alipangiwa kufanyakazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, na kuhudumu katika wizara kwa zaidi ya miaka 35.

''Nimehudumu katika awamu zote sita za serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, nikiwa katika wizara hiyo hiyo kwa kweli nilipata bahati na heshima ya kuweza kuaminiwa…..wengine wanasema ni kama nilizaliwa Wizara ya Mambo ya nje, kukulia humo na kuzeekea humo….'' Anasema Balozi Mulamula huku akicheka.

Anasema katika kipindi hicho chote cha utendaji kazi mambo meng amekutana nayo mazuri kwa mabaya,

(Anacheka) ''..Yaani kwa kweli ni mengi labda niseme ya furaha, sitaki ya masikitiko. ya furaha ni kwamba mimi nimepata teuzi mbalimbali na faraja zaidi katika historia ya wizara hiyo ni mimi peke yangu niliyeanzia chini kama ofisa na nikapita ngazi zote mpaka nikawa Katibu na baadaye waziri kwenye wizara hiyo, kwa hiyo ni furaha yangu kwa vile sio wengi wanaopata bahati hiyo, nashukuru kwa kuaminiwa na kuweza kupanda vyeo.''

Kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa balozi na Rais wa awamu ya tatu marehemu Benjamin Mkapa, kusimamia idara ya ya Ushirikiano wa kimataifa, wizarani ya mambo ya nje.

''Nilikuwa mwanamke peke yangu kati ya walioteuliwa ubalozi wakati huo, kwa hiyo hata ukiona picha iliyopigwa, peke yangu ndio utaona nimevaa kitenge, kila nikiangalia hiyo picha napata faraja kubwa kwa kweli. Na hiyo ilikuwa mwaka 2004.'' Alisema balozi Mulamula.

Katika utendaji wake wa kazi akiwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje anasema wakati mwingine alijikuta akipewa majukumu makubwa na wakati mwingine akiona kama anaelemewa lakini hakuwa na budi kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa.

''Kwa mfano nilivyoteuliwa kwa Katibu Mtendaji wa kwanza nchi za maziwa mkuu- lilikuwa jukumu kubwa sana, lakini nikalibeba nikafanya kazi, changamoto zilikuwa nyingi sana unajua katika hali ya machafuko katika kanda yetu na kila mtu alikuwa akiniangalia mimi ….Kwa hiyo kila wakati ilikuwa kichwani mwangu, kwamba nisishindwe, nisishindwe, nisiwaangushe viongozi wangu ambao wameniamini kwamba kazi hiyo naiweza''

Lakini pia katika nafasi nyingine alizoteuliwa balozi Mulamula anasema aliteuliwa bila ya kuambiwa, (Hakuandaliwa). Akitolea mfano uteuzi wake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya nchi za Nje.

''Wakati nilipokuwa Balozi Marekani niliteuliwa kuwa Katibu mkuu , nikasema naanzia wapi kuibeba wizara, watu kwanza wanakuwa hawaamini huyu kweli kachaguliwa kuwa katibu mkuu, kwa hiyo kwanza unatakiwa kuondoa hisia hiyo…. Lakini majukumu ya Katibu mkuu wa Wizara ni makubwa sana, yanataka maamuzi yanahitaji rasilimali- rasilimali watu, rasilimali pesa… huna pesa…huna wafanyakazikwa hiyo kwa kweli mimi nadhani kazi ya Katibu mkuu ilikuwa ni changamoto kuliko kazi zote nilizowahi kufanya katika wizara hiyo.

Kuitumikia kwake Tanzania katika Umoja wa Mataifa pia kulimpa nafasi ya kuweza kubobea zaidi katika masuala ya diplomasia fani yake aliyoisomea chuoni.

''Kama mtu yoyote anataka kuwa mwana diplomasia ni vizuri akawa pale umoja wa mataifa kwa vile ni shule kubwa sana, maana ni kama dunia yote inakuwa katika kiganja chako. Unaelewa siasa za mataifa yote… unaelewa ulimwengu ukoje... Diplomasia ya ulimwengu iko pale katika umoja wa mataifa. Na uzuri Tanzania ilikuwa na sauti, siasa yetu ya mambo ya nje ilituweka mahali pazurii. Uzuri wa Tanzania ilikuwa na sauti, sisi pamoja na udogo wetu kama nchi lakini tulikuwa na sauti, hata ukiwa kama afisa mdogo ukiongea kama Tanzania kila mtu anakusikiliza… amenieleza balozi Mulamula.

Akizungumzia hali ya kisiasa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Balozi Liberata Mulamula licha ya kwa sasa nchini mwake kuwa ni Mbunge wa kuteuliwa, lakini pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wanawake katika Umoja wa Nchi za Afrika -AU anaamini kwamba amani ya kudumu haiwezi kuletwa na nchi za nje, japo kuwa zinasaidia lakini jukumu lote ni la wa Afrika weyewe.

''Ndio maana unaona wakati ule Rais Samia akaitisha mkutano wa viongozi wa Afrika masharaiki na nchi za SADC kuzungumzia mzozo wa Congo ni ile hali ya kwamba jukumu liwe letu… Lakini sasa ndio limeondoshwa na huku mapigano yanaendelea.. Hali hiyo inanisikitisha.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI