MBEYA. Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya Frank Mwaisumbe, amechukua fomu ya kuomba kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Mbeya mjini akisema ndiye mwenye uwezo wa kuwa msemaji na mtetezi wa wananchi juu ya kero zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, Mwaisumbe amesema ameamua kuomba nafasi ya kugombea ubunge wa Mbeya mjini kurithi mikoba ya Dkt. Tulia Ackson aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kabla ya kutangaza kwenda kugombea jimbo la Uyole.
Amesema jiji la Mbeya linaendelea kupiga hatua kimaendeleo na kwa lilipofikia linahitaji mtu mahiri wa kuendelea kusemea changamoto za wananchi hasa katika mhimili wa bunge hivyo kueleza kuwa na uwezo usiokuwa na mashaka na ushawishi Serikali ili kuwapigania wananchi endapo atapata nafasi hiyo.
Frank Mwaisumbe ambaye awali alishawahi kuwa Mtumishi wa umma Serikalini pia amempongeza mtangulizi wake katika jimbo hilo Dkt. Tulia Ackson kwa kuendelea kuwa sauti ya wananchi wa Mbeya mjini kabla ya jimbo hilo kugawanywa na hivyo amesema ikiwa atapitishwa na chama chake kuwa mgombea ubunge Mbeya mjini ataeleza bayana vipaumbele vyake na namba atakavyopambana kuwapigania wananchi.
MWISHO.
0 Comments