Header Ads Widget

ENG. KUNDO ALILIWA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA BARIADI MJINI.

 

Katibu Mwenezi kutoka Kata ya Mhango, Lucas Hazina, (aliyesimama) akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani), akiwa na Makatibu Wenezi wenzake wa CCM kutoka Kata za Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi. 


MAKATIBU wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutoka Kata 10 za Halmashauri ya Mji wa Bariadi zinazounda Jimbo la Bariadi Mjini, wamemtaka Mhandisi Kundo Mathew kugombea nafasi ya Ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi utakaofanyika Mwezi Oktoba mwaka huu.



Itakumbukwa kuwa, Mhandisi Kundo ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mkoani Simiyu lililokuwa linaundwa na Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya wilaya ya Bariadi.


Wakizungumza leo na waandishi wa Habari, Makatibu Wenezi hao wamesema wanatambua namna Mbunge huyo alivyotekeleza na kusimamia miradi ya Maendeleo ndani ya miaka mitano kwenye kata 31 zilizokuwa zinaunda Jimbo la Bariadi.


Katibu Mwenezi kutoka Kata ya Mhango, Lucas Hazina amesema baada ya Jimbo la Bariadi kugawanywa, Mbunge huyo alitangaza kugombea Ubunge Jimbo la Bariadi vijijini huku baadhi ya watu (akiwemo Masanja Kadogosa), wakionyesha nia ya kugombea Jimbo hilohilo badala ya kugawanywa.


"Siku za kuchukua fomu zimekaribia, Kwa umoja wetu tumekubaliana na tunamwomba Mhandisi Kundo agombee Jimbo la Bariadi Mjini lenye kata 10...Maombi yetu makubwa ni kumwomba Mhandisi Kundo arudi kugombea Jimbo la Bariadi Mjini, hakuna haja ya kufuatana na Kadogosa kwenda kuvurugana huko" ameeleza Mwenezi huyo.


Ameeleza kuwa, "hakuna sababu ya kufuatana na kugombea eneo moja maana watakigawa Chama cha Mapinduzi...Wenezi wa Jimbo la Bariadi Mjini kwa Umoja wetu tumekubaliana kumwomba agombee Jimbo la Bariadi mjini".



Amesema Mbunge huyo amewafanyia mambo makubwa ikiwemo kuwapatia usafiri wa pikipiki na baiskeli kwa makatibu kata na wa Matawi pamoja na kukiwezesha Chama.


Ameongeza kuwa, Makatibu hao wako tayari kumchangia fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu za kugombea nafasi ya Ubunge wa jimbo hilo ili aweze kuwatumikia wananchi kwa miaka mitano ijayo.


Maria Biseko, Katibu Mwenezi wa Kata ya Malambo, amesema wananchi wa Kata ya Malambo wanamhitaji Mhandisi Kundo aendelee kuwatumikia kutokana na kusimamia vizuri miradi ya Maendeleo katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Umeme na Barabara.


Simbayu Kuselya, Katibu Mwenezi wa Kata ya Nyakabindi, wamekubalina na wanamlilia Mhandisi Kundo agombee Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini kutokana na kumsaidia Rais Dk. Samia kusimamia miradi ya Maendeleo ikiwemo Mradi wa Maji wa ziwa Victoria wenye gharama ya shilingi Bil. 440 akiwa Naibu Waziri wa Maji.


"Tunamuomba sana Mhandisi Kundo agombee Ubunge wa Jimbo la Bariadi, na mimi ninatoa hapa shilingi 100,000/= kumchangia achukue fomu na wenezi wenzangu tutahakikisha tunachanga na kufikisha shilingi Mil.1" amesema.


Kija Mathias, Katibu Mwenezi wa Kata ya Bariadi, amesema wenezi hao wameshakubaliana na wanamtaka Mhandisi Kundo agombee Jimbo la Bariadi mjini licha ya kutangaza kugombea Jimbo la Bariadi vijijini.



Aidha, Makatibu wenezi hao wamesema watambua mchango wake baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bariadi mwaka 2020 ambapo aliachangia mifuko ya saruji 150 Kwa kila kata ili kujenga ofisi za Chama Cha Mapinduzi ngazi za Kata pamoja na kugawa usafiri ili kuwezesha watendaji wa Chama kufanya kazi.


Mwisho.

Katibu Mwenezi kutoka Kata ya Mhango, Lucas Hazina akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) kwa lengo la kumtaka Mhandisi Kundo kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Bariadi Mjini.


Simbayu Kuselya, Katibu Mwenezi wa Kata ya Nyakabindi, akiwaonyesha kiasi cha shilingi 100,000/=  ili kumchangia Mhandisi Kundo ili aweze kuchukua fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini.


Maria Biseko, Katibu Mwenezi wa Kata ya Malambo akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) kwa lengo la Kumtaka Mhandisi Kundo Mathew kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Bariadi Mjini.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI