NA MATUKIO DAIMA MEDIA,MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Juma Zuberi Homera, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutekeleza kwa haraka ujenzi wa barabara ya mchepuo kutoka Mbalizi hadi Iyunga, ili iweze kutumika kwa magari makubwa, huku magari madogo yakielekezwa kutumia barabara kuu ya sasa. Hatua hiyo inalenga kupunguza ajali zinazochangiwa na msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Dkt. Homera ametoa agizo hilo leo, alipowasili katika eneo la ajali lililopo Mlima Iwambi, , ambapo ajali mbaya imesababisha vifo vya watu 28 na kujeruhi wengine 9. Ajali hiyo imehusisha lori lenye namba za usajili T.830 EDP na T.148 CTD, ambalo lilishindwa breki na kugonga magari mawili — daladala na gari dogo aina ya Kirikuu.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa TANROADS kuhakikisha barabara ya mchepuo inakamilika haraka ili magari makubwa yatumie njia hiyo, na barabara ya sasa ibaki kwa ajili ya magari madogo pekee,” amesema Dkt. Homera.
Ameongeza kuwa serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wote waliolazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi, pamoja na kutoa rambirambi ya shilingi 500,000 kwa kila familia iliyofiwa. Serikali pia itasimamia maandalizi ya majeneza kwa miili yote 28.
Dkt. Homera amewatembelea majeruhi hospitalini na kuzungumza na familia zilizofika kwa ajili ya utambuzi wa miili ya ndugu zao. Ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kuwa na subira wakati huu mgumu, akisisitiza kuwa serikali iko pamoja nao na itaendelea kushughulikia kila hatua.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo ni uzembe wa dereva wa lori hilo. Licha ya kuwa miongoni mwa majeruhi, dereva huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Aidha, Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa madereva wote kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima, ambazo husababisha maafa na maumivu makubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.
0 Comments