Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza na Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Urekebu, Ahmad Mwen-dadi, amesema kuwa mafunzo wanayopewa wafungwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha wafungwa wanapata stadi za kazi zitakazowawezesha kujitegemea na kujipatia kipato mara baada ya kumaliza vifungo vyao.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremia Yolamu Katungu, Kamishna Mwen-dadi amesema lengo ni kuhakikisha kuwa wanaomaliza vifungo vyao wanarejea katika jamii wakiwa na maarifa ya kuwaondoa katika mnyororo wa uhalifu.
Katika hatua nyingine, Kamishna huyo amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya magereza 129 nchini yanatumia nishati safi, jambo linalosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni. Hatua hiyo pia ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa taasisi zote zenye zaidi ya watu 100 kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya kila siku.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Juma Homera, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuyatumia vyema maarifa waliyopata, na kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu pindi watakapomaliza vifungo vyao.
Malisa ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Magereza ili kuhakikisha dhamira ya urekebishaji kwa wafungwa inafikiwa kwa vitendo, akisisitiza kuwa mafanikio ya urekebishaji yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za serikali na jamii kwa ujumla.
0 Comments