Header Ads Widget

WIKI YA MAZIWA KITAIFA MOROGORO

 

Na Lilian Kasenene,Morogoro 

KATIKA kuelekea maadhimisho ya wiki ya maziwa kitaifa, watanzania wametakiwa kutumia Elimu inayotolewa na wataalaamu juu ya umuhimu wa unywaji wa maziwa ili kupata lishe bora.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya 28 ya wiki ya maziwa yanayoadhimishwa kitaifa  mkoani Morogoro kuanzia Mei 27 hadi Juni mosi Mwaka huu katika uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha ndege maeneo ya Fire katika  manispaa ya Morogoro.

Kutokana na umuhimu wa maziwa alisema ni vyema kukawepo kwa sera ya umuhimu wa tasnia ya maziwa ambayo itawafanya wazalishaji wa maziwa kufuga kwa ufanisi ng'ombe wa maziwa ili kufikia malengo ya kukuza uchumi.

Aidha mkuu huyo wa mkoa alisema kwa sasa Tanzania inakadiriwa mtu mmoja amekuwa  akinywa lita 67 za maziwa kwa mwaka ukilinganisha na nchi nyingine kama Kenya ambapo unywaji ni lita 130 na Uganda lita 70.

"Huko Duniani watu wanakunywa maziwa lita 360,370,kwa  nchi zinazoongoza kwa unywaji maziwa,lakini Afirika pekee inazalisha asilimia tatu(3)tu ya maziwa yanayozalishwa duniani ukilinganisha na nchi ya India   ambaye ndie mzalishaji namba Moja yeye anachangia asilimia 25,hivyo Bodi ya maziwa lazima iangalie fursa ya uzalishaji iliyopo kwa wafugaji,"alisema.

Alieleza kuwa wiki ya maziwa itatumika kuwaelimisha wafugaji na watanzania juu ya ufugaji kibiashara ambao utamfanya kukua kiuchumi kwa kufuga ng'ombe wa kisasa wawe wa upandikizaji ama njia nyingine na wenye tija.

"Kuna fursa kubwa kwa wafugaji,na masoko yapo Afrika,hili jambo la kuongeza uzalishaji wa maziwa linkwenda sambamba na kuelimishana, ni lazima tuweke mikakati,"alisema 

Wakati ambao bado sekta hiyo ya maziwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji mdogo na kiwango Cha chini Cha unywaji wa maziwa akashauri wafugaji kuwa na jukwaa Moja la kuwakutanisha ili kuambizana mambo yanayowakabili na namna ya kuyatatua.

Malima alisema katika wiki hiyo kutakuwa na ugawaji wa maziwa kwenye vituo vya watoto yatima, Hospitali, pamoja na Magereza.

Mwakilishi wa msajili wa Bodi ya maziwa ambaye ni afisa masoko wa Bodi hiyo Said Isike alizungumzia Maendeleo ya program ya unywaji maziwa mashuleni ambapo alisema program hiyo bado inatekelezwa nchini katika mikoa 45, ambapo kwa Morogoro zipo shule mbili za msingi za Mafiga na mchikichini kwa wanafunzi kupata maziwa kwa bei nafuu.

Akasema katika shule hizo, kuna shule 5 ambazo zimefungiwa mashine maalum za kuuzia maziwa ATM, na kwamba bado kuna changamoto ya upungufu wa maziwa na uhaba wa mashine hizo ingawa bado program hiyo ni endelevu.

Isike alisema lengo la program  hiyo ni kuwafanya wanafunzi kuwa na tabia ya kupenda kunywa maziwa Kila wakati.

Mteknolojia wa chakula katika Bodi hiyo Rajilan Hilali alisema katika ukanda wa kitropiki na joto lililopo uzalishaji wa maziwa bado ni changamoto,hivyo kutokana na hali hiyo katika ukanda huo akashauri ufugaji wa ng'ombe chotara ili kupata walau wastani wa lita 10 hadi 15 kwa siku.

"Kwa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya ndo unaweza kupata maziwa lita 20 kutokana na ukanda wa hali ya hewa kuwa baridi,"alisema Hilali.

Maadhimisho hayo yatafanyika Mei 27 Hadi Juni 1,2025 katika viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro na yatakwenda sambamba na  shughuli mbalimbali yakilenga kuhamasisha matumizi na uzalishaji wa maziwa

Kauli mbili ni 'Maziwa Salama kwa Afya Bora na uchumi endelevu,'


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI