Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia jumla ya watu 57 kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu, ikiwemo wizi, uvunjaji, na umiliki haramu wa silaha, katika msako maalum unaoendelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi, amethibitisha kukamatwa kwa watu wanne waliokuwa wakimiliki silaha aina ya bastola (pisto) kinyume na sheria.
Watuhumiwa hao walinaswa katika maeneo ya Dodoma mjini na Wilayani Mpwapwa wakiwa na silaha za kienyeji Wilayani Mpwapwa zinazotumia risasi aina ya shotgun, wakihusishwa na uhalifu katika maeneo mbalimbali.
Katika tukio tofauti lililotokea Mei 18 2025 usiku, maeneo ya Kizota, watuhumiwa wawili walikamatwa wakisafirisha mafuta lita 2,420 bila vibali halali. Mafuta hayo yanahisiwa kuwa ya wizi na uchunguzi wa kina unaendelea.
“Katika operesheni hii, tumefanikiwa pia kuwakamata watuhumiwa 57 wa makosa ya wizi na uvunjaji. Kati yao, 27 tayari wamefikishwa mahakamani, huku 30 wakiendelea kuhojiwa,” alisema SACP Katabazi.
Vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kutumika katika uhalifu pia vimekamatwa, ikiwa ni pamoja na runinga 6, redio 7, pamoja na vifaa 30 vingine vya kuvunjia.
WITO KWA WANANCHI
SACP Katabazi ametoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuhakikisha wanazikabidhi kwa hiari kupitia ofisi za serikali za mitaa au vijiji kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Msako bado unaendelea. Tunawaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu au umiliki haramu wa silaha. Ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kulinda amani na usalama,” alisisitiza Kamanda Katabazi
Mwisho
0 Comments