Shirika la haki za binadamu nchini India linachunguza ripoti kwamba zaidi ya watoto 100 waliugua kwa kula chakula cha mchana shuleni baada ya nyoka aliyekufa kupatikana kwenye chakula hicho.
Inasemekana mpishi huyo bado alitoa chakula hicho cha mchana licha ya kumuondoa mnyama huyo kutoka ndani ya sufuria, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (NHRC) ilisema kwenye taarifa.
Tume hiyo ilisema takriban watoto 500 wanaaminika kupewa chakula hicho katika mji wa Mokama katika jimbo la Bihar, mashariki mwa India.
Baada ya watoto kuanza kuugua, wenyeji walifunga barabara na kufanya maandamano, NHRC ilisema.
“Tume imeona yaliyomo, ikiwa ni kweli, yanaibua suala kubwa la ukiukwaji wa haki za binadamu za wanafunzi,” ilisema.
Taarifa hiyo ilidai "ripoti ya kina" ndani ya wiki mbili kutoka kwa maafisa wakuu wa serikali ambayo itajumuisha "hali ya afya ya watoto".
Mnamo mwaka 2013, chakula kilichokuwa na sumu kilisababisha vifo vya watoto 23 wa shule katika jimbo la Bihar.
Polisi walisema viwango vya juu vya "sumu" viligunduliwa wakati wa utafiti wa kisayansi.
0 Comments