Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju ametoa wito kwa Waratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kuhakikisha wanaimarisha uratibu na utekelezaji wa mpango huo katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Akizungumza katika kikao kazi cha waratibu wa MTAKUWWA kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kilicholenga kuwapatia Mafunzo kuhusu uratibu na utekelezaji wa Mpango Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya St. Gasper jijini Dodoma kinalichoanza Mei 28 hadi 31 , 2025, Mpanju amesema kikao hicho ni muhimu katika kujenga uelewa kuhusu uratibu wa MTAKUWWA II (2024/25 – 2028/29)
Wakili Mpanju amesema Waratibu wa MTAKUWWA ni kiungo muhimu katika kuhakikisha afua za mpango huo zinatekelezwa kikamilifu na ni lazima wasimame imara, washirikiane na maafisa wa mikoa, halmashauri na wadau wote ili kuandaa na kusimamia mipango mikakati ya utekelezaji wake
Aidha, amesisitiza kuwa Mpango huo unalenga kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake, watoto na jamii kwa ujumla huku akisisitiza kila mkoa kuhakikisha unaandaa mpango mkakati wake wa utekelezaji wa MTAKUWWA
Pia amesisitiza utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango huo huku akiwasihi kusimamia na kushauri katika utengaji wa Bajeti kwaajili ya utekelezaji wa Mpango huo katika maneno yao.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamiii Patrick Golwike amewataka Waratibu hao kwenda kutumia elimu waliyoipata katika mafunzo hayo kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mpango huo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa weledi ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Katika kikao hicho washiriki ambao ni waratibu wa MTAKUWWA kutoka mikoa yote 26 walieleza kuwa kikao hicho kimewajengea uelewa wa kina kuhusu wajibu wao na namna bora ya kuendesha shughuli za uratibu na kueleza kuwa kupitia majadiliano ya pamoja na miongozo waliyopewa sasa wana uwezo wa kuratibu kwa ufanisi afua za kupambana na ukatili katika jamii.
Aidha, wameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa na Serikali kupitia Wizara yamepokelewa kwa uzito mkubwa na kwa pamoja wameahidi kwenda kuyatekeleza kwa vitendo mara watakaporejea katika maeneo yao ya kazi.
0 Comments