Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amewataka wanafunzi 120 wa shule za msingi kutoka wilaya hiyo wanaokwenda kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa kwa mwaka 2025, kuzingatia nidhamu, maadili na juhudi kubwa ili kuiletea heshima wilaya yao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wanamichezo hao iliyofanyika mjini Same, Mhe. Kasilda alisema mashindano hayo ni fursa adhimu kwa watoto kuonesha vipaji vyao, lakini pia ni jukwaa la kukuza nidhamu, ushirikiano na uzalendo miongoni mwao.
“Nendeni mkashindane kwa bidii na mkiwa na nia ya kuibuka washindi. Kumbukeni kuwa mnaibeba wilaya nzima, hivyo mnapaswa kujiepusha na tabia zozote hatarishi zitakazoharibu maisha yenu au sifa ya shule zenu,” alisema Mhe. Kasilda.
Aliongeza kuwa mafanikio katika mashindano ya mkoa si tu yataleta heshima kwa Same, bali yatafungua milango kwa wachezaji chipukizi kuchaguliwa kuiwakilisha mkoa ngazi ya kitaifa. Aidha, aliahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kukuza michezo wilayani humo.
Miongoni mwa wadau waliojitokeza kudhamini maandalizi ya timu hiyo ni Benki ya NMB, ambayo imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo vikiwemo mipira, jezi, viatu na soksi kwa wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo.
Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Meneja wa NMB Tawi la Same, Saad Masawila, alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua sekta ya michezo kuanzia ngazi ya shule za msingi.
“Tunaamini kwamba michezo ni sehemu muhimu ya malezi bora kwa watoto wetu. Kwa kusaidia maandalizi ya mashindano kama haya, tunachangia kuibua vipaji ambavyo vitakuja kulitumikia taifa katika siku za usoni,” alisema Masawila.
Aliongeza kuwa NMB itaendelea kuwa mdau wa maendeleo ya jamii kwa kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na michezo, huku akitoa wito kwa mashirika mengine kujitokeza kusaidia vipaji vya watoto wa Kitanzania.
0 Comments